IQNA

Kuchomwa moto Qur’ani kutavuruga uhusiano wa Uislamu na Ukristo

12:10 - September 09, 2010
Habari ID: 1991044
Jumuiya ya Makanisa ya Kiprotestanti ya Indonesia (PGI) imelaani hatua ya kanisa la Marekani ya kutangaza tarehe 11 Septemba kuwa ni siku ya kimataifa ya kuchoma moto Qur’ani na kusema kuwa hatua hiyo itachafua uhusiano kati ya Uislamu na Ukristo.
Jumuiya ya Makanisa ya Kiprotestanti ya Indonesia imemtumia barua ya wazi Rais Barack Obama wa Marekani ikisisitiza kuwa kitendo hicho kitazusha mivutano kati ya Waislamu na Wakristo katika pembe mbalimbali duniani.
Viongozi wa Kikristo wa Indonesia pia wamesisitiza katika barua hiyo kwamba kuchomwa moto kitabu kitukufu cha Qur’ani kutazirejesha jamii nyuma katika kipindi cha karne za kati na kwenye vita dhidi ya ustaarabu. Vilevile wamemtaka kiongozi huyo wa Marekani akabiliane na hatua hiyo ya madharau.
Jumuiya ya Makanisa ya Kiprotestanti ya Indonesia inawakilisha zaidi ya makanisa elfu 20 na Wakristo milioni 9. Zaidi ya asilimia 85 ya jamii ya watu wa Indonesia ni wafuasi wa dini ya Kiislamu na nchi hiyo ndiyo yenye jamii kubwa zaidi ya Waislamu duniani.
Ni vyema kukumbusha hapa kuwa kasisi Terry Jones wa kanisa moja la Florida nchini Marekani ametoa wito wa kuainishwa tarehe 11 Septema kuwa siku ya kimataifa ya kuchomwa moto kitabu cha Qur’ani. Kasisi huyo ni miongoni mwa maadui wakubwa wa dini ya Kiislamu nchini Marekani na amewataka wafuasi wa kanisa lake kuchoma moto kitabu kitakatifu cha Qur’ani Jumamosi ijayo ya tarehe 11 Septemba ikiwa ni sehemu ya kukumbuka mashambulizi ya Septemba 11 mwka 2001 katika miji ya New York na Washington. 651025

captcha