Ahmad al-Misrawi, Sheikh al-Qurra wa Misri au kwa ibara nyingine shekhe wa wasomaji Qura'ni wa Misri amesisitiza juu ya udharura wa kuimarishwa shule za mafunzo ya Qur'ani Tukufu na kushiriki wasomaji mashuhuri wa Qur'ani katika mafunzo ya shule hizo.
Kwa mujibu wa tovuti ya Rosaonline.net Sheikh al-Misrawi amesema kuwa shule za mafunzo ya Qur'ani katika vijiji vya Misri zimepungua sana ikilinganishwa na miaka ya huko nyuma na kwamba zimepoteza nafasi zilizokuwa nayo katika mfumo wa mafunzo ya Qur'ani.
Amesema shule hizo zilikuwa na nafasi muhimu katika utoaji mafunzo ya Qur'ani na hasa katika mwezi Mtukufu wa Ramadhani ambapo wasomaji mashuhuri wa Qur'ani walikuwa wakishiriki na kutoa mchango wao katika ufundishaji Qur'ani katika shule hizo, jambo ambalo liliwanufaisha wengi.
Sheikh al-Misrawi amesema kwa masikitiko kwamba, hii leo shule hizo zimepoteza nafasi hiyo kutokana na kudhihiri televisheni za kawaida na za satalaiti ambazo zimedhoofisha nafasi halisi ya shule hizo. Al-Masrawi amesema zamani washindani wa Qur'ani wa Misri walikuwa wakipewa zawadi nyingi katika mashindano ya Qur'ani lakini kwamba hii leo nchi hiyo imepoteza nafasi hiyo kutokana na kuchaguliwa watu wasiofaa kushiriki katika mashindano ya kimataifa katika nchi tofauti.
Amesema mwishoni kwamba, katika miaka ya hivi karibuni Walibya wamekuwa wakiimarisha nafasi yao katika mashindano ya kimataifa ya usomaji Qur'ani. 657416