IQNA

Ratiba ya duru ya utangulizi ya mashindano ya Qur'ani Afrika Kusini kutangazwa

12:54 - September 23, 2010
Habari ID: 1999873
Ratiba ya washiriki wa duru ya utangulizi ya mashindano ya Qur'ani Tukufu ya Afrika Kusini tayari imeainishwa na Tasisi ya Qur'ani ya Afrika Kusini na washiriki watatangaziwa ratiba hiyo hii leo Alkhamisi.
Muntaha Ibrahim Kani, mkuu wa taasisi hiyo ambaye pia anasimamia mashindano hayo amesema katika mahojiano na shirika la habari za Qur'ani IQNA kwamba leo Alkhamisi washiriki wa mashindano hayo watatangaziwa ratiba ya aya watakazotakiwa kusoma katika mashindano hayo, ikiwa ni siku moja kabla ya kuanza kwake rasmi. Amesema mashindano hayo ambayo yatawashirikisha karibu watu 20 katika kila kundi yatafanyika katika makundi matatu ya wanaume ya watoto, vijana na watu wazima.
Kani amesema kuwa marefa wa mashindano hayo ambao wanatoka katika nchi za Malaysia, Indonesia na Afrika Kusini watawachagua watu watano katika kila kundi ambao hatimaye watashiriki katika hatua ya mwisho ya mashindano hayo ambayo yamepangwa kufanyika Jumapili tarehe 26 Septemba.
Washindi wa duru hiyo ya mwisho watachaguliwa na kupewa vibali vya kuwawezesha kushiriki katika mashindano ya kimataifa kama wawakilishi wa Afrika Kusini. Amesema mashindano hayo ambayo yalianza kuandaliwa Afrika Kusini mwaka 2005 mwanzoni yalifanyika katika kiwango cha mkoa wa Cape Town tu lakini hatimaye yakafanywa kuwa ya kitaifa mwaka uliofuata wa 2006.
Bwana Kani amesema kuwa mbali na kuandaa mashindano ya Qur'ani, Tasisi ya Qur'ani ya Afrika Kusini ambalo ni shirika lisilokuwa la kiserikali linajishughulisha kuendesha masomo ya usomaji Qur'ani kwa makundi yote ya wanaume na wanawake. 660720
captcha