IQNA

Malaysia kuwa mwenyeji wa kongamano la kimataifa la utafiti wa Qur’ani

18:00 - November 01, 2010
Habari ID: 2023725
Kongamano la kwanza la kimataifa la utafiti wa Qur’ani limepangwa kufanyika tarehe 11 na 12 Januai mwakani katika mji wa Kuala Lumpur nchini Malaysia.
Kongamano hilo litasimamiwa na Kituo cha Utafiti wa Qur’ani na Kitengo cha Utafiti wa Qur’ani na Hadithi cha Chuo Kikuu cha Utafiti wa Kiislamu cha Malaya. Lengo la kongamano hilo limetajwa kuwa ni kutayarisha uwanja wa kubadilisha maarifa kati ya watafiti, wanachuo na wanafikra katika nyanja za ufafiti wa sayansi ya Qur’ani.
Malengo mengine ya kongamano hilo la kimataifa yametajwa kuwa ni kuanzisha kanali ya mawasiliano kwa ajili ya utafiti wa Qur’ani, kuchunguza nyanja mbalimbali za utafiti wa Qur’ani na kupanua zaidi utafiti huo, kutayarisha fusra za kuchunguza tafiti zinazofanywa na wasomi, kuwakutanisha pamoja watafiti na kutumia teknolojia katika kueneza elimu na maarifa ya Qur’ani.
Maudhui za kongamano hilo ni pamoja na nafasi na mchango wa vituo vya vyuo vikuu na taasisi mbalimbali katika kutoa huduma za Kiqur’ani, mchango wa maulamaa katika tafsiri ya Qur’ani Tukufu, sheria na vigezo katika Qur’ani, hakika ya muujiza wa kitabu hicho cha mbinguni, thamani za kibinadamu katika Qur’ani na utumiaji wa teklonojia ya kisasa katika kuhudumia Qur’ani.
Makala zitakazoshinda katika kongamano hilo zitachapishwa katika jarida la Kituo cha Utafiti wa Qur’ani cha Chuo Kikuu cha Malaya.
Kituo cha Utafiti wa Qur’ani cha Malaya ndicho kituo cha kwanza cha utafiti wa masuala ya Qur’ani na Uislamu nchini Malaysia. Kituo hicho kiliasisiwa mwanzoni mwa mwaka huu katika chuo hicho kikuu cha kale zaidi nchini Malaysia. 686509

captcha