Baraza la Maulamaa wa Kishia la Bahrain limetangaza kuwa limeamua kuuita mwaka mpya wa Hijria Qamariya kuwa mwaka wa kuwa pamoja na Qur'ani kufuatia hujuma zinazofanywa na maadui wa umma wa Kiislamu dhidi ya kitabu kitakatifu cha Qur'ani.
Taarifa iliyotolewa na Baraza la Maulamaa wa Kishia la Bahrain imesema kuwa maadui wa umma wa Kiislamu wanataka kuchafua mafundisho ya dini hiyo na kuzima nuru ya kitabu cha Mwenyezi Mungu lakini njama hizo zote zimefeli. Imeongeza kuwa la kusikitisha zaidi ni kunyamaza kimya Waislamu na kutoipa umuhimu Qur'ani Tukufu, suala ambalo linawavimbisha kichwa maadui.
Baraza la Maulama wa Kishia la Bahrain limesema, kwa msingi huo kaulimbiu ya mwaka mpya wa Hijria Shamsia itakuwa "kuwa pamoja na Qur'ani" ili Waislamu wote washikamane na kitabu hicho cha Mwenyezi Mungu, wakikitetee na kueneza nuru yake.
Taarifa ya Baraza la Maulamaa wa Kishia la Bahrain imemalizia kwa kusisitiza juu ya udharura wa kushirikiana matabaka yote ya jamii kwa ajili ya kufanikisha kaulimbiu hiyo. Vilevile limewataka Waislamu wote kufanya jitihada za kuimarisha mafundisho ya Qur'ani katika umma wa Kiislamu. 690474