IQNA

Nchi za Kiafrika zinashika rekodi ya kushinda mashindano ya Qur’ani Saudi Arabia

8:24 - January 05, 2011
Habari ID: 2059039
Mashindano ya 32 ya kimataifa ya kuhifadhi, tajwidi na tafsiri ya Qur’ani yamemalizika nchini Saudi Arabia huku wawakilishi wa nchi za Kiafrika wakishika nafasi nyingi zaidi za juu za mashindano hayo.
Shirika la habari la Saudia limeripoti kuwa sherehe za kutuzwa washindi wa mashindano ya kimataifa ya Saudi Arabia zilifanyika Jumapili iliyopita katika ukumbi wa Ismail Abu Daud mjini Jiddah na kwamba majina ya wawakilishi wa nchi za Nigeria, Algeria, Libya, Niger na Morocco yalionekana kwa wingi zaidi kati ya majina 25 ya makarii waliofanya vizuri zaidi katika mashindano hayo.
Katika uwanja wa kuhifadhi Qur’ani nzima pamoja na tafsiri ya kitabu hicho, Abdullah al Qarafi wa Saudi Arabia alishika nafasi ya kwanza akifuatiwa na makarii wanne kutoka nchi tofauti za Kiafrika.
Katika uwanja wa hifdhi ya Qur’ani pamoja na tajwidi, Muhammad Bakr Zarami Yusuf kutoka Nigeria alishika nafasi ya tatu akifuatiwa na Ahmad Muhammad Shahbun kutoka Morocco.
Katika hifdhi ya juzuu 20 pamoja na tilawa na tajwidi, Ibrahim Sonusi kutoka Libya alishika nafasi ya tatu.
Ripoti zinasema kuwa wanaharakati 70 wa masuala ya Qur’ani kutoka nchi mbalimbali wamehudhuria katika mashindano ya 32 ya kimataifa ya Qur’ani ya Saudi Arabia, na mwishoni washiriki 25 waliarifishwa kama washindi. Baada ya Afrika, wawakilishi wa Saudi Arabia, Bangladesh, Uturuki, Yemen na Kuwait pia walishika nafasi nzuri katika mashindano hayo. 723998
captcha