Ghana, nchi ya Kiafrika yenye watu wa dini tofauti wanaoishi pamoja kwa amani, inakabiliwa na uhaba wa walimu hodari wa lugha ya Kiarabu kwa ajili ya wanafunzi wa Qur'ani.
Hayo yamesemwa na Othman Abdullah Paty mwakilishi wa Ghana katika Mashindano ya Kimataifa ya Qur'ani ya Wanachuo Waislamu yaliyomalizika hivi karibuni nchini Iran. Ameiambia IQNA kwamba kunafanyika juhudi za kuondoa nakisi hiyo na kwamba walimu hodari wa lugha ya Kiarabu kutoka nchi za Misri na Saudi Arabia wanatumwa nchini Ghana kwa ajili ya kufunza Kiarabu na sayansi ya Qur'ani.
Hafidhi huyo wa Qur'ani kutoka Ghana amelaani vitendo vya maadui wa Uislamu vya kuvunjia heshima kitabu hicho kiakatifu na akasema kwa mujibu wa aya ya 9 ya suratul Hijr, Mwenyezi Mungu mwenyewe ameahidi kukilinda kitabu hicho.
Othman Abdullah Paty ameashiria pia hadithi za Bwana Mtume zinazohimiza kuhifadhi Qur'ani na akasema kwa mujibu wa hadithi hizo watu waliohifadhi Qur'ani ndio watakaokuwa wa kwanza kuingia peponi baada ya Mitume wa Mwenyezi Mungu.
Othman Abdullah mbaye amehifadhi Qur'ani nzima anasema, nchini Ghana darsa za Qur'ani hufanyika wakati wa ibada za Magharibi na Ishaa.
Karii huyo wa Ghana amesifu mashindano ya kimataifa wa Qur'ani ya wanachuo Waislamu yaliyofanyika nchini Iran na akasema kuwa amefaidi mno kwa kushiriki katika mashindano hayo. 733753