Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kila mwaka inaonyesha tukio muhimu la kiutamaduni na Kiislamu katika eneo la Mashariki ya Kati kwa kuitisha mashindano ya kimataifa ya Qur'ani na mashindano hayo huwa ni medani ya kuthibitisha nafasi ya juu ya Iran katika hifdhi na kiraa ya Qur'ani Tukufu.
Hayo yamesemwa na Hussain Hamdan mwanachama wa jopo la majaji wa Mashindano ya 28 ya Kimataifa ya Qur'ani Tukufu yanayoendelea hapa mjini Tehran. Ameongeza kuwa mashindano ya Qur'ani yanayofanyika kila mwaka yakiwashirikisha wawakilishi wa zaidi ya nchi 60 yanabainisha uhusiano wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na kitabu cha Mwenyezi Mungu na yanaonyesha kwamba nchi hii inashikamana barabara na Qur'ani Tukufu.
Hussein Hamdan ambaye ni jaji wa mashindano ya Qur'ani kutoka Lebanon amesema kuwa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran chini ya uongozi wa Ayatullah Ali Khamenei kila mwaka hutayarisha mashindano ya Qur'ani ya kiwango cha juu kwa ajili ya kuarifisha nafasi ya kitabu hicho cha Mwenyezi Mungu kwa walimwengu na kutangaza kuwa Iran iko mstari wa mbele katika masuala ya Qur'ani.
Kuhusu kushiriki kwake katika jopo la majaji wa mashindano ya sasa ya kimataifa ya Qur'ani mjini Tehran Hussein Hamdan amesema: :Hii ni mara yangu ya pili kushiriki katika Mashindano ya Kimataifa ya Qur'ani ya Tehran kama jaji na mara yangu ya kwanza ilikuwa mwaka 2008 wakati nilipokuja Iran katika mashindano ya Qur'ani ya wanafunzi wa vyuo vikuu.
Karii huyo wa Lebanon amesema, washindani wa siku ya pili ya mashindano haya ya Qur'ani walikuwa bora zaidi ya wale waliosoma siku ya kwanza. Ameongeza kuwa japokuwa mashindano haya hayajafikia mwisho, lakini hadi sasa wasomi wa Iran wamefanya vizuri zaidi na wameweza kuthibitisha nafasi ya juu ya Iran katika medani ya kiraa na hifdhi ya Qur'ani Tukufu. 818721