IQNA

Waislamu Kenya watakiwa kuwasaidia wasiojiweza mwezi wa Ramadhani

12:35 - July 12, 2011
Habari ID: 2153151
Shirika la Tabligh ya Kiislamu la Bilal (Bilal Muslim Mission) nchini Kenya limetoa wito kwa Waislamu wanaojiweza nchini humo kutoa misaada kwa wale wasiojiweza katika mwezi mtukufu wa Ramadhani.
Katika taarifa yake iliyotolewa kupitia tovuti ya intaneti ya kenbilal, Shirika la Tabligh ya Kiislamu la Bilal limesema bei ya bidhaa za vyakula imepanda sana na vilevile kuna baadhi ya maeneo ya Kenya yaliyo na uhaba wa chakula. Kutokana na hali hiyo kuna baadhi ya familia ambazo haziwezi kupata chakula cha kila siku. Watoto ndio walioathiriwa zaidi.
Huku Waiislamu nchini Kenya wakijitayarisha kuukaribisha mwezi mtukufu wa Ramadhani, wametakiwa kuwakumbuka wasiojiweza kwa kuhakikisha kuwa hawakosi chakula cha iftari na daku.

Shirika la Tabligh ya Kiislamu la Bilal limesema litatoa misaada katika Misikiti 26 katika maeneo ya vijijini na vile vile kuzisaidia familia 3,169 za vijijini na mijini katika Mwezi wa Ramadhani. Aidha shirika hilo pia litapeleka misaada ya chakula kwa Waislamu katika shule za sekondari za Kiislamu na magereza .
Itakumbukwa kuwa Umoja wa Mataifa umetangaza kuwa mamillioni ya watu katika nchi za Somalia, Djibouti, Ethiopia na Kenya wanakabiliwa na baa la njaa. Nchi hizo zimekubwa na ukame mkubwa zaidi ambao haujawahi kushuhudiwa katika kipindi cha miaka 60 iliyopita.
Aghalabu ya watu wanaokumbwa na njaa katika nchi hizo ni Waislamu.
Katika upande mwingine Shirika la Tabligh ya Kiislamu la Bilal limesema litakuwa na vipindi maalumu vya radio katika mwezi mtukufu wa Ramadhani.
824320
captcha