IQNA

Baraza la Kiislamu Zimbabwe lalaani kuuawa kigaidi Luteni Jenerali Qassem Soleimani

15:03 - January 13, 2020
Habari ID: 3472369
TEHRAN (IQNA) – Baraza Kuu la Masuala ya Kiislamu Zimbabwe limelaani vikali hatua ya Marekani kutekeleza hujuma ya kigaidi na kumuua Luteni Jenerali Haj Qassem Soleimani na wanamapambano wenzake hasa Abu Mahdi al Muhandis.

Kwa mujibu wa mwandishi wa IQNA, Mwenyekiti wa Baraza Kuu la Masuala ya Kiislamu Zimbabwe  Sheikh Ismail Duwa ametuma barua rasmi kwa Ubalozi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran mjini Harare ambapo ametuma salamu za rambirambi kwa Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu na taifa la Iran kufuatia jinai ya kigaidi ya Marekani ya kumuua Luteni Jenerali Qassem Soleimani na Wenzake. Huku akilaani vikali jinai hiyo, ameongeza kuwa: "Si mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran pekee uliompoteza kamanda huyo shujaa aliyekuwa anapigania amani, bali ulimwengu mzima na hasa Waislamu ndio ambao wamepata pengo kubwa baada ya kuuawa jenerali huyo."

Aidha Sheikh Duwa mfume wa ubeberu duniani umewalenga Waislamu wote duniani kwa kumuua kigaidi Luteni Jenerali Qassem huku akisisitiza umuhimu wa Waislamu wa madhehebu ya Shia na Sunni kulinda umoja wao ili kuutetea Uislamu.

Sheikh Duwa pia ametoa wito kwa makhatibu wa Sala ya Ijumaa katika miji yote mikubwa nchini humo kuakisi kadhia ya ugaidi huo wa Marekani na kuulani vikali katika hotuba zao ikiwa ni katika kumuenzi Shahidi Luteni Jenerali Qassem Soleimani.

Luteni Jenerali Qassem Soleimani, Kamanda wa Kikosi cha Quds cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu IRGC, Ijumaa Alfajiri 3 Januari aliwasili nchini Iraq kufuatia mwaliko rasmi wa wakuu wa nchi hiyo. Punde baada ya kuwasili, akiwa ndani ya gari pamoja na Abu Mahdi al Muhandis, Naibu Kamanda wa kikosi cha kujitolea cha wananchi wa Iraq maarufu kama al Hashd al Shaabi pamoja na watu wengine nane, walishambuliwa kwa anga na wanajeshi vamizi na wa kigaidi wa Marekani karibu na uwanja wa ndege wa Baghdad na wote walikufa shahidi katika tukio hilo.

Kufuatia ugaidi huo wa Marekani usiku wa kuamkia Jumatano 8 Januari, Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu IRGC lilizipiga kwa makumi ya makombora, kambi mbili za Marekani nchini Iraq ikiwa ni kujibu jinai ya kigaidi iliyiofanywa na askari vamizi wa Marekani ya kumuua shahidi Luteni Jenerali Qassem Soleimani, Kamanda wa Kikosi cha Quds cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu IRGC.

3871044/

captcha