IQNA-Watu wasiopungua 94 wameuawa shahidi na makumi ya wengine kujeruhiwa kufuatia mashambulio mawili ya kigiadi katika mji wa Kerman kusini mashariki mwa Iran. Taarifa zinasema yamkini idadi ya waliofariki na majeruhi ikaongezeka.

Ripoti zimebaini kuwa, milipuko miwili mikubwa imetokea leo katika mji wa Kerman kwenye njia inayoelekea katika makaburi ya mashahidi mjini Kerman.
Milipuko hiyo imetokea wakati watu walipokuwa wakielekea katika makaburi hayo ya mashahidi kwa ajili ya hauli na kumbukumbu ya mwaka wa nne wa kuuawa shahidi Luteni Jenerali Qassem Soleimani.
Taarifa zaidi zinasema kuwa, milipuko hiyo pacha imetokea jirani makaburi ya mashahidi mjini Kerman ambapo ndipo lilipo kaburi la shahidi Qassem Soleimani.
Maafisa wa usalama wamesem tukio hilo ni hujuma ya kigaidi iliyowalenga watu wasio na hatia yoyote. Hadi sasa hakuna kundi lililotangaza kuhusika na hujuma hiyo ya kigaidi.
Kulingana na IRNA, mlipuko wa kwanza ulitokea umbali wa mita 700 kutoka kwenye kaburi la Shahidi Luteni Jenerali Soleimani na mlipuko wa pili umbali wa kilomita moja.
Shirika la habari la Tasnim lilitaja vyanzo ambavyo havikutajwa vikisema kuwa mifuko miwili iliyosheheni vilipuzi ambayo ililipuliwa kwa mbali ndiyo iliyosababisha milipuko hiyo. IRNA pia ilinukuu chanzo cha habari kikisema mifuko miwili ya mabomu iliyolipuliwa na rimoti ilisababisha milipuko hiyo.
Mlipuko wa kwanza ulitokea saa nane na dakika hamsini kwa saa za Iran. La pili lilifanyika dakika 10 baadaye, kulingana na Meya wa Kerman Saeed Tabrizi, ISNA iliripoti.
Shirika la Hilali Nyekundu la Iran limesema waokoaji wake watatu waliuawa na mlipuko wa pili.
3486673