IQNA

Israel yaua na kujeruhi Wapalestina 150 katika 'mitego ya kifo' ya vituo vya misaada Gaza

12:16 - June 01, 2025
Habari ID: 3480773
IQNA-Ofisi ya Habari ya Serikali katika Gaza imetangaza kuwa wanajeshi wa utawala wa Kizayuni wa Israel wamefanya mauaji mapya ya halaiki dhidi ya raia wa Kipalestina katika maeneo ya usambazaji wa misaada ya kibinadamu, ambayo yanajulikana kama “mitego ya kifo”, ambapo watu wasiopungua 30 wameuawa shahidi na zaidi ya 120 kujeruhiwa.

Ibrahim Abu Saoud, ambaye alishuhudia shambulizi la Israel dhidi ya watu wanaotafuta misaada karibu na Rafah, amesema wanajeshi wa Israel waliwafyatulia risasi watu waliokuwa wakielekea kwenye kituo cha usambazaji misaada ya kibinadamu kinachoungwa mkono na utawala huo wa Kizayuni.

"Kulikuwa na watu wengine waliouawa shahidi, wakiwemo wanawake", Abu Saoud, 40, amenukuliwa akisema na shirika la habari la Associated Press. Ameeleza kuwa, "Tulikuwa karibu mita 300 kutoka kwa jeshi la Israel."

Abu Saoud amesema aliona watu wengi wakiwa na majeraha ya risasi, akiwemo kijana mmoja ambaye aliripotiwa kufariki dunia katika eneo la tukio. "Hatukuweza kumsaidia," ameongeza.

Wakati huo huo, Mkurugenzi wa huduma za ambulensi huko Gaza amezungumza na Al Jazeera kuhusu shambulio hilo, na masuala mapana yanayokabili huduma za ambulensi katika eneo la hilo pwani.

Amesema vikosi vya Israel vinazuia magari ya kubebea wagonjwa kufika eneo kulikojiri shambulio la bomu mjini Rafah, ili kutoa msaada kwa waliojeruhiwa.

Kwa mujibu wa afisa huyo, wahudumu wa afya wanahatarisha maisha yao ili kuwaokoa waliojeruhiwa kutokana na shambulio la bomu la Israel huko Rafah.

Ameongeza kuwa, vituo vya usambazaji wa misaada katika Ukanda wa Gaza vimekuwa vituo vya udhalilishaji, na jumuiya ya kimataifa lazima ivizuie.

Tangu kuanza kwa vita vya Gaza mwezi Oktoba 2023, Ukanda wa Gaza umekuwa chini ya mzingiro mkali uliowekwa na utawala wa Kizayuni, hali ambayo imesababisha uhaba mkubwa wa chakula, maji, dawa na mafuta, na hivyo kuisukuma hali ya kibinadamu katika eneo hilo kuelekea baa la njaa.

Hii ni licha ya onyo la mara kwa mara kutoka kwa Umoja wa Mataifa na mashirika ya haki za binadamu kuhusu kuzorota kwa hali ya kibinadamu na hatari ya kutokea kwa njaa ya kiwango kikubwa katika Gaza. Viongozi wa Palestina na baadhi ya taasisi za kimataifa wamemtuhumu utawala wa Tel Aviv kwa kutumia njaa kama silaha ya kivita.

285760

Habari zinazohusiana
Kishikizo: gaza jinai za israel
captcha