IQNA-Rais Gustavo Petro wa Colombia amelaani kimya kinachoonyeshwa kwa vita vya kinyama vinavyoendelezwa na utawala wa Kizayuni wa Israel katika Ukanda wa Ghaza, na kusisitiza kwamba mauaji ya kimbari yanafanyika huko Palestina.

Katika ujumbe alioweka kwenye mtandao wa kijamii wa X, Petro amesema: "mtu yeyote anayetetea mauaji haya ya kimbari au kukaa kimya mbele ya mauaji hayo ameharibu hali yake ya ubinadamu".
Rais wa Colombia ameendelea kubainisha: "inaonekana kana kwamba (waziri wa propaganda wa Nazi Joseph) Goebbels ndiye anayeongoza mawasiliano ya dunia ili makumi ya maelfu ya waandishi wa habari wanyamazishwe mbele ya wenzao waliouawa na watoto 20,000 walioraruliwa vipande-vipande na mabomu".
Petro amelaani pia kitendo cha jeshi la utawala wa Kizayuni cha kuvamia ofisi ya kituo cha habari cha televisheni ya Al Jazeera hapo jana katika mji wa Ramallah ulioko Ukingo wa Magharibi, ambapo jeshi hilo liliamuru ofisi hiyo kufungwa kwa siku 45.
Rais wa Colombia ametoa kauli hiyo siku moja baada ya Mjumbe Maalum wa Marekani wa Kufuatilia na Kupambana na chuki dhidi ya Wayahudi, Deborah Lipstadt, kumlaumu Petro kwa msimamo wake wa kukosoa mashambulizi ya kinyama ya jeshi la Israel katika Ukanda wa Gaza.
Katika jibu lake kwa mwanadiplomasia huyo wa Marekani, Rais Petro ameandika kwenye X: "Bibie Balozi, Wapalestina ni Wasemiti...Ni kuonyesha chuki dhidi ya Wayahudi kuua watoto kwa kurusha mabomu huko Ghaza na sio kuupinga. Suala la kuonyesha chuki dhidi ya Wayahudi leo hii ni kurudia mauaji aliyofanya Hitler dhidi ya ubinadamu na hasa kwa watu wa Palestina".
3489999