IQNA

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu

Ulaya imefungamana na vikwazo vya Marekani dhidi ya Iran, tusiwe na matumaini nayo

18:11 - September 26, 2019
Habari ID: 3472148
TEHRAN (IQNA) - Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitiza namna malengo ya uadui wa nchi za Ulaya dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu kimsingi yasivyo na tofauti na ya adui Marekani na kueleza kuwa: Nchi za Ulaya kidhahiri zinajidhihirisha kuwa patanishi na kusema maneo mengi lakini yote hayo ni maneno matupu.

Ayatullah Sayyed Ali Khamenei Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameyasema hayo Alhamisi  asubuhi mjini Tehran alipokutana na kufanya mazungumzo na wajumbe wa Baraza la Wanavyuoni Wataalamu Linalomchagua Kiongozi Muadhamu. Katika kikao hicho amewasilisha tathmini yake ya kina kuhusu hali ya nchi na kuimarika shaari na nguvu ya kimapinduzi na kisiasa ya mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu katika eneo. Amekutaja kustafidi na darsa za kipindi cha kujitetea kutakatifu na kuenea kwake katika jamii kuwa ni jambo lenye umuhimu mkubwa. Kiongozi Muadhamu amesisitiza kuwa, maendeleo endelevu ya nchi yanahitajia, kumtegemea Mwenyezi Mungu, kusimama kidete na kuendeleza muqawama na mapambano, kuwa na matumaini na mustakbali, kuwaamini vijana khususan vijana wanamapinduzi, kuweko umoja na mshikamao wa matabaka tofauti ya wananchi khususan miongoni mwa wanamapinduzi, kuunga mkono kwa dhati uzalishaji wa ndani na kukata kikamilifu utegemezi na kuwatumainia maajinabi.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu aidha amesisitiza kuwa njia ya kuamiliana na kufanya mazungumzo na nchi nyingine yoyote isipokuwa Marekani na utawala wa Kizayuni haijafungwa na kuongeza kuwa: Licha ya hayo kivyovyote vile hatupasi kuziamini nchi zilizobeba bendera ya uadui dhidi ya mfumo wa Kiislamu; zikiongozwa na Marekani na nchi kadhaa za Ulaya kwa sababu nchi hizo zinalifanyia uadui waziwazi taifa la Iran. 

Ayatullah Khamenei ameashiria pia utendaji wa nchi za Ulaya baada ya kufikiwa makubaliano ya nyuklia na nchi hizo kutotekeleza ahadi zao, hasa baada ya Marekani kujitoa kwa upande mmoja katika makubaliano ya JCPOA na kurejeshwa vikwazo vya kidhulma vya nchi hiyo dhidi ya Iran; na kuongeza kuwa: Nchi za Ulaya zimeendelea kufungamana na vikwazo vya Marekani licha ya ahadi zao na hazijachukua hatua yoyote katika uwanja huo; na baada ya hapo pia haitazamiwi kwamba zitachuka hatua yoyote kwa maslahi ya Jamhuri ya Kiislamu. Kwa msingi huo, tunapasa kuondoa kabisa matumaini kwa nchi za Ulaya.

3845075

 

captcha