IQNA

Kiongozi Muadhamu
20:32 - October 02, 2019
News ID: 3472156
TEHRAN (IQNA) - Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameashiria kufeli siasa za Marekani za kuiwekea Iran mashinikizo ya juu zaidi na kutosalimu amri Tehran mbele ya mashinikizo hayo ya mfumo wa kibeberu na kusisisitiza kuwa, Iran itaendelea kwa nguvu zote kupunguza ahadi zake ndani ya mapatano ya nyuklia ya JCPOA hadi itakapofikia lengo lililokusudiwa.

Ayatullah Sayyid Ali Khamenei amesema hayo leo (Jumatano) wakati alipoonana na maelfu ya makamanda wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu. Amegusia pia juhudi njama zilizofeli hivi karibuni za Marekani za kujaribu kuonesha kuwa Iran imeshindwa na imesalimu amri mbele ya mashanikizo hayo na kuongeza kuwa, Wamarekani wamefikia hata kumbembeleza kwa kila namna Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ili akubali kuonana nao na wawaoneshe walimwengu kuwa Iran imeshindwa na imesalimu amri. Ameongeza kuwa, "wamefikia hata kutumia marafiki wao wa Ulaya lakini hadi hivi sasa wameshindwa na napenda kukuhakikishieni kuwa kamwe hawatofanikiwa."

Kiongozi Muadhamu amebaini kuwa, suala la kupunguza ahadi za nyuklia limo mikononi mwa Shirika la Nishati ya Atomiki la Iran na hivyo shirika hilo linapaswa kuendelea kutekeleza kazi hiyo vilivyo, kwa kina na kikamilifu yale yote yanayotangazwa na serikali hadi yatakapopatikana matunda yaliyokusudiwa na bila ya shaka yoyote matunda hayo yatapatikana.

Ayatullah Khamenei amezungumzia pia hasara kubwa wanayopata maadui hasa Marekani huko Afghanistan, Iraq na Syria na kusisitiza kuwa, mabeberu wametumia fedha nyingi kuunda genge la Daesh (ISIS) na kuliunga mkono kikamilifu kisilaha, kifedha na kipropaganda, lakini hivi sasa kutokana na hima ya vijana wa Syria, Iraq na Iran, genge la Daesh limeangamizwa, lakini utawasikia mabeberu hao wanaeneza uongo wakidai kuwa eti wao ndio walioliangamiza genge hilo.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amepongeza uwezo wa majimui adhimu ya muqawama katika kupambana na kambi ya kufru na dhulma na kutoa nasaha kwa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) akisema: Hakikisheni mnaulinda mtazamo wenu mpana unaoangalia hadi nje ya mipaka ya Iran kuhusu jiografia ya kambi ya muqawama.

Ayatullah Khamenei pia amesema: "Katika kila mtazamo unaoangalia mapambano ya taifa la Iran na ulimwengu wa dhulma, uistikbari na kufru, inabainika kuwa, taifa la Iran hatimaye litapata ushindi."

3846644

Name:
Email:
* Comment:
* captcha: