IQNA

Sanaa ya Kiislamu Imejikita ndani ya Nyoyo na Imani za Watu wa Iran

9:02 - March 01, 2011
Habari ID: 2088202
Ayatullah Udhma Sayyid Ali Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, akizungumza katika sherehe za kuzindua zulia lenye thamani kubwa lililonakshiwa juzuu zote 30 za Qur'ani Tukufu, amesema kwamba sanaa ni matunda ya kazi za mwanaadamu.
Ameongeza kuwa sanaa inayoundika kutokana na ilhamu ya ndani ya nafsi na kuchirizika kutoka katika kipaji cha kimaanawi cha mwanaadamu na wakati sanaa hiyo inapotoka ndani ya nyoyo na imani sahihi kwa maana halisi ya neno, hapo ndipo huweza kuitwa sanaa ya Kiislamu.
Kiongozi Muadhamu amesema hayo katika mkutano wake na Rais wa Chuo Kikuu cha Sanaa za Kiislamu cha Tabriz mkutano ambao umehudhuriwa pia na manaibu, jopo la wahadhiri wa chuo hicho na wakuu wa vitivo mbali mbali vya sanaa vya Chuo Kikuu hicho ambapo katika mkutano huo, limeonyeshwa pia kwa mara ya kwanza zulia lenye thamani kubwa lililonakshiwa juzuu zote 30 za Qur'ani Tukufu.
Ayatullah Udhma Khamenei amesema kwamba zulia hilo lenye thamani kubwa ni fakhari ya kubakia milele na ni kumbukumbu adhimu sana kwa ajili ya mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na kwamba kazi hiyo imetokana na mapenzi makubwa waliyo nayo wasanii wa Iran. Amesema jina na kumbukumbu za waliofuma zulia hilo zitabakia hai kwa karne nyingi.
Vile vile amewashukuru wasanii wote waliofanikisha kazi hiyo kubwa ya lisanii na kusisitiza kwamba inabidi zulia hilo litolewe zawadi kwa Haram ya Imam Ridha AS ili liweze kubakia huko daima na kuweza kuwanufaisha watu wote.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema pia kwamba suala la sanaa ya Kiislamu ni muhimu mno na huku akiashiria juu ya tofauti iliyopo baina ya sanaa ya Kiislamu na sanaa zisizo za Kiislamu amesema kwamba, roho ya sanaa ya Kiislamu ndiyo inayotofautisha sanaa hiyo na sanaa zisizo za Kiislamu kwani sanaa ni kazi ya mkono wa mwanaadamu inayotokana na ilhamu yake ya ndani na kuundika kwa michirizo ya kimaanawi na wakati sanaa hiyo inapotoka ndani ya moyo na kwenye imani sahihi kwa maana halisi ya neno, hapo huitwa sanaa ya Kiislamu.
Ayatullah Udhma Khamenei ameongeza kuwa, haiwezekani kuunda sanaa ya Kiislamu kwa amri na kushinikiza ila wakati roho, moyo na mtazamo wa msanii unapokuwa sahihi, matokeo ya mtazamo wa msanii huyo huzaa sanaa ya Kiislamu.
Vile vile amesema ni jambo la dharura kuzingatiwa sanaa za mikono katika maeneo tofauti ya Kiislamu na ameusia kuhamasishwa walimu na watu walioko mstari wa mbele katika kazi hiyo ili sanaa za mikono ambazo kwa kawaida ni kazi zenye mashaka na usumbufu mwingi ziweze kuendelea na kunawiri zaidi.
Mwanzoni mwa mkutano huo, Dk. Kiinejad, Rais wa Chuo Kikuu cha Sanaa za Kiislamu cha Tabriz ametoa ripoti fupi kuhusiana na kazi za Chuo Kikuu hicho na kusema kuwa, Chuo Kikuu cha Sanaa za Kiislamu kina kozi 22 za Shahada ya Kwanza, kozi 10 za Shahada ya Pili na kozi mbili za Shahada ya Udaktari na kwamba katika kipindi cha miaka 11 tangu kuanza kufanya kazi chuo hicho hadi hivi sasa, kimeweza kustafidi na walimu wengi wenye uzoefu ambao wana uwezo mkubwa katika kuhuisha sanaa za jadi nchini.
755545
captcha