IQNA

Mjumbe wa Jihad Islami: Shahidi Soleimani aliwaunganisha wapigania ukombozi Palestina

16:13 - January 13, 2021
Habari ID: 3473552
TEHRAN (IQNA) - Mwakilishi wa harakati ya Jihadul Islami ya kupigania ukombozi wa Palestina nchini amepongeza nafasi ya Luteni Jenerali Shahidi Qassem Soleimani katika kuwaunganisha Wapalestina.

Ameongeza kuwa: "Shahidi Soleimani aliyaunganisha na kuyaimarisha makundi ya muqawama ya Palestina mbele ya utawala wa Kizayuni."

Akizungumza Jumanne hapa Tehran katika mahojiano na Shirika la Habari la Iran Press, Nasser Abu Sharif  ameeleza kuwa: Shahidi Soleimani aliunga mkono muqawama na mapambano dhidi ya mabeberu na akasema: "Harakati za mapambano ya Kiislamu (Muqawama) hazingeweza kukabiliana na kusimama kidete mbele ya mashambulizi hatari ya Wazayuni na Marekani kama isingekuwa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Haj Qassem Soleimani, wanajihadi wenzake na uungaji wao mkono usio na ukomo.  

Abu Sharif ameongeza kuwa: Shahidi Soleimani alikuwa na nafasi kuu katika kuunganisha na kuimarisha ari ya mhimili wa muqawama; na hilo ndilo lililoimarisha nguvu ya mhimili wa muqawama mkabala wa utawala Kizayuni na njama za Magharibi. 

Mwakilishi wa harakati ya Jihadul Islami ya Palestina hapa Tehran amezungumzia pia mazoezi ya karibuni ya makundi ya muqawama ya Palestina huko Ghaza na ujumbe wake na kueleza kuwa: Maneva hayo ya karibuni yaliyofanyika sambamba na kumbukumbu ya kutimia mwaka mmoja tangu kuuliwa kigaidi Haj Qassem Soleimani yamedhihirisha umoja uliopo baina ya makundi ya muqawama mkabala na utawala wa Kizayuni. 

Luteni Jenerali Qassem Soleimani, Kamanda wa Kikosi cha Quds cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) alielekea Iraq Januari 3 mwaka 2020 kufuatia mwaliko rasmi wa wakuu wa Iraq.

Punde baada ya kuwasili Iraq aliuawa shahidi katika hujuma ya ndege za kivita za jeshi vamizi na la kigaidi la Marekani karibu na uwanja wa ndege wa Baghdad. Aidha katika hujuma hiyo ya kigaidi Abu Mahdi Al Muhandis, Naibu Mkuu wa Harakati ya Kujitolea ya Wananchi wa Iraq, naye pia aliuawa shahidi akiwa ameandamana na Qassem Soleimani. Watu wengine wanane waliokuwa katika msafara huo nao pia waliuawa shahidi.

Shahidi Luteni Jenerali Qassem Soleimani alikuwa na nafasi kubwa katika mapambano na maadui pamoja na magaidi na pia katika kuangamiza kundi la kigaidi la Daesh au ISIS. Pia alikuwa nguzo muhimu katika harakati za kupigania ukombozi wa Palestina. Halikadhalika alikuwa na nafasi muhimu katika kusambaratisha njama ya Marekani na Wazayuni ya kuligawa eneo vipande vipande.

3947376

captcha