IQNA

Sayyid Hassan Nasrallah

Shahidi Soleimani aliwatetea Waislamu na hata wasiokuwa Waislamu wakiwemo Wakristo

23:47 - January 03, 2021
Habari ID: 3473521
TEHRAN (IQNA)- Katibu Mkuu wa Harakati ya Hizbullah ya Lebanon amesema Shahidi Qassem Soleimani hakuwa ni mtetezi wa Waislamu wa madhehebu ya Shia pekee bali aliwatetea Waislamu wote na hata wasiokuwa Waislamu wakiwemo Wakristo na alijitolea muhanga kwa ajili yao.

Sayyid Hassan Nasrallah ameyasema hayo Jumapili usiku katika hotuba ambayo ameitoa kwa mnasaba wa kuwadia mwaka moja tokea wauawe shahidi Luteni Jenerali Qassem Soleimani Kamanda wa Kikosi cha Quds cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) na Abu Mahdi al Muhandis, Naibu Mkuu wa Kikosi cha Kujitolea cha Wananchi wa Iraq maarufu kama Al Hashd al Shaabi. Katika hotuba yake, Sayyid Nasrallah amesema Shahidi Soleimani aliunga mkono kikamilifu harakati za muqawama au mapambano ya Kiislamu katika eneo la Asia Magharibi. Ameongeza kuwa dhulma aliyotendewa Shahidi Soleimani na wanamapambano wenzake itabakia katika historia.

Katibu Mkuu wa Hizbullah ameongeza kuwa, Iran inamtambua Shahidi Soleimani kama bingwa na shujaa wa kitaifa nao watu wa Lebanon na Hizbullah inamtambua kama shujaa na bingwa aliyejitolea muhanga, mtiifu na mwenye kutetea waliodhulimiwa katika ulimwengu wa Kiislamu. Amesema Shahidi Soleimani hakuwa ni mtetezi wa Waislamu wa madhehebu ya Shia pekee bali aliwatetea Waislamu wote na hata wasiokuwa Waislamu wakiwemo Wakristo na alijitolea muhanga kwa ajili yao.

Sayyid Hassan Nasrallah amebaini kuwa, Shahidi Luteni Soleimani alikuwa shujaa na bingwa wa dunia ambapo harakati zote za kupigania uhuru na ukombozi zinamtazama kama kigezo. Aidha amesema mbali na Shahidi Solemani  mashahidi Abu Mahdi al Muhandis, Haj Imad Mughniya, Sayyid Mustafa Badruddin na makamanda wa muqawama huko Palestina na Lebanon pia ni vigezo.

Katibu Mkuu wa Hizbullah amesema mafanikio ya Shahidi Soleimani yalikuwa mengi sana na kuongeza kuwa, leo mataifa ya eneo na harakati za muqawama na mapambano ya Kiislamu zimetangaza utiifu wao kwa mashahidi na makamanda wa muqawama.

Sayyid Hassan Nasrallah amesisitiza kuwa, mauaji ya Shahidi Soleimani na Shahidi Al Muhandis daima yatabakia katika fikra za umma na kuongeza kuwa, wakati wowote itakapo, na bila kuhitajia waitifaki wake wa eneo, Iran inaweza kulipiza kisasi mauaji ya Luteni Jenerali Qassem Soleimani.

Aidha kiongozi huyo wa Hizbullah amesema Marekani ilidhani kwa kumuua Shahidi Soleimani muungano wa harakati za mapamabano ya Kiislamu ungesambaratika lakini hilo halikutokea.

Amesema kila wakati harakati za mapamabano ya Kiislamu zinapopoteza kamanda, huibuka zikiwa na nguvu na irada imara zaidi na hivyo amesema wote wanapaswa kufuata njia ya makamanda wa muqawama katika kutetea umma wa Kiislamu.

Luteni Jenerali Qassem Soleimani, Kamanda wa Kikosi cha Quds cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) alielekea Iraq Januari 3 mwaka 2020 kufuatia mwaliko rasmi wa wakuu wa Iraq.

Punde baada ya kuwasili Iraq aliuawa shahidi katika hujuma ya ndege za kivita za jeshi vamizi na la kigaidi la Marekani karibu na uwanja wa ndege wa Baghdad. Aidha katika hujuma hiyo ya kigaidi Abu Mahdi Al Muhandis, Naibu Mkuu wa Harakati ya Kujitolea ya Wananchi wa Iraq, naye pia aliuawa shahidi akiwa ameandamana na Qassem Soleimani. Watu wengine wanane waliokuwa katika msafara huo nao pia waliuawa shahidi.

Shahidi Luteni Jenerali Qassem Soleimani alikuwa na nafasi kubwa katika mapambano na maadui pamoja na magaidi na pia katika kuangamiza kundi la kigaidi la Daesh au ISIS. Pia alikuwa nguzo muhimu katika harakati za kupigania ukombozi wa Palestina. Halikadhalika alikuwa na nafasi muhimu katika kusambaratisha njama ya Marekani na Wazayuni ya kuligawa eneo vipande vipande.

3945469

captcha