IQNA

Rouhani: Marekani haina budi ila kulipigia magoti taifa la Iran

18:12 - March 01, 2021
Habari ID: 3473693
TEHRAN (IQNA) - Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema Marekani haina budi ila kulipigia magoti taifa la Iran baada ya kukiri kufeli sera zake za vikwazo.

Rais Hassan Rouhani ameyasema hayo leo wakati alipohutubu katika ufunguzi wa miradi mikubwa ya sekta za mafuta na gesi na kuongeza kuwa: "Kwa yakini dunia na Marekani haitakuwa na budi ila kupiga magoti mbele ya taifa la Iran na kuondoa vikwazo vya kidhalimu."

Aidha amesema kukiri serikali ya Marekani kuhusu kufeli mashinikizo na vikwazo vyake dhidi ya Iran ni mafanikio makubwa kwa taifa la Iran. Rais wa Iran amesisitiza kuwa,  "Kile ambacho tumeweza kukipata ni kutokana na irada, imani na kusimama kidete wananchi."

Rais Rouhani ameongeza kuwa serikali mpya ya Marekani hadi sasa imekiri mara nne kuwa 'mashinikizo ya juu kabisa' dhidi ya Iran yamefeli na hayajazaa matunda. Ameongeza kuwa kukiri huko ni mafanikio makubwa katika historia kwani wale ambao wameiwekea Iran vikwazo wanakiri wazi kuwa  kutofika popote  vikwazo hivyo.

Rais Rouhani ameshiriki kwa njia ya video katika uzinduzi wa mradi wa kisima kikubwa cha mafuta cha Azar Ilam magharibi mwa Iran ambacho kina uwezo wa kuzalisha mapipa 65,000 ya mafuta ghafi ya petroli kwa siku. Aidha alizindua mradi wa kiwanda cha usafishaji mafuta cha  Kangan kusini mwa Iran na pia mradi wa shirika la petrokemikali la Kian katika eneo la Assaluyeh.

Iran inaendelea kuzindia miradi mikubwa ya mafuta na gesi kwa kutegemea wataalamu wa ndani ya nchi na hivyo kupelekea vikwazo vya Wamagharibi na hasa Marekani dhidi ya nchi hii kufeli.

3956931

captcha