IQNA

Rais wa Iran asisitiza kuhusu Marekani kufidia makosa iliyoyafanya

23:48 - March 16, 2021
Habari ID: 3473741
TEHRAN (IQNA)- Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa kufidia makosa yaliyofanywa na serikali iliyopita ya Marekani si kwa manufaa ya Iran tu bali ni kwa maslahi ya Marekani yenyewe , eneo na taasisi za kimataifa.

Akizungumza leo katika hafla ya uzinduzi wa miradi mbalimbali ya sekta ya maji na nishati ya Iran, Rais Hassan Rouhani amesema kuwa kuzinduliwa miradi hiyo katika kipindi hiki kigumu cha vita vya kiuchumi na maambukizi ya corona kumeonyesha kuwa wananchi wa Iran, vijana na wahandisi wa Kiirani wapo hai. Ameongeza kuwa serikali mtenda jinai ya Marekani imelifanyia dhulma kubwa taifa la Iran kutokana na mipango yake ya ugaidi. 

Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran aidha amebainisha kuwa, serikali ya sasa ya Marekani imekiri mara kadhaa kwamba hatua zlizochukuliwa na serikali ya kabla yake zilikuwa makosa, hata hivyo baada ya kupita miezi miwili hatujaona hatua zozote za kivitendo zikichukuliwa ili kufidia makosa hayo ya Marekani; bali yamekuwa ni maneno matupu, na tunataraji kuwa watarejea katika njia ya busara na kufuata sheria. 

Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema, mwaka huu ulikuwa mwaka mgumu kwa wananchi adhimu wa Iran na kwamba aghalabu ya shughuli za kiuchumi na mchakato wa uuzaji nje na uingizaji bidhaa wa nchi hii umekumbwa na matatizo na hata ununuaji wa chanjo ya corona umathiriwa na vizuizi kutokana na kuendelea hatua za kigaidi za uingiliaji wa Marekani.

3960128

captcha