IQNA

15:08 - November 10, 2026
Habari ID: 3483023

Jinsi Msikiti wa Jordan unavyotumia tena maji ya udhu katika bustani

IQNA – Katika mojawapo ya nchi zenye uhaba mkubwa wa maji duniani, msikiti mmoja nchini Jordan umebuni njia ya kipekee ya kuhifadhi rasilimali, kwa kusafisha maji yanayotumika kwa udhu na kuyaelekeza kumwagilia bustani zake.

Abu Obeida Mosque

Msikiti wa Abu Obeida katika mji wa Deir Alla, mkoa wa Balqa magharibi mwa Amman, uko katika mojawapo ya maeneo yenye joto kali na ukame zaidi katika Bonde la Jordan. Licha ya mazingira kame yanayouzunguka, msikiti huo umezungukwa na miti, vichaka na vitalu vya maua vinavyostawishwa kwa mfumo wa umwagiliaji wa matone.

Maji hayo hayatoki kwenye mabomba ya manispaa. Badala yake, hukusanywa kutoka kwenye mabomba yanayotumiwa na waumini kuosha mikono, nyuso na miguu yao kabla ya swala.

Waislamu hutawadha, yaani kujitoharisha kwa kuosha viungo kunakohitajika kabla ya swala, mara tano kwa siku. Nchini Jordan, ambako upatikanaji wa maji safi ni mita za ujazo 61 tu kwa kila mtu kwa mwaka, kila tone lina thamani. Kiwango hiki ni cha chini mno ya kizingiti cha Umoja wa Mataifa cha uhaba kamili wa maji, ambacho ni mita za ujazo 500 kwa kila mtu.

Ahmed al-Rawsan, mwanzilishi wa Chama cha Uhifadhi wa Maji cha Jordan (JACA), kinachosimamia mfumo wa kuyatumia tena maji wa msikiti huo, anasema mpango huo unaonyesha jinsi taasisi za kidini zinavyoweza kutekeleza maadili ya mazingira kwa vitendo.

Mfumo huo hufanya kazi kupitia mabomba yaliyowekwa chini ya eneo la udhu la msikiti. Maji yaliyotumika hukusanywa na kuhamishiwa kwenye kitengo cha kusafisha, ambako hupita katika tabaka tano za changarawe na mchanga kabla ya kuelekezwa bustanini.

“Watu hapa wanaelewa uhaba wa maji kwa sababu wanauishi kila siku,” anasema al-Rawsan. Anaongeza kuwa kutokuwepo kwa sabuni wakati wa udhu kunarahisisha kiasi mchakato wa kusafisha, kwa kuwa maji hayo hayana kemikali zinazoweza kuutatiza.

Mpango huo unakuja wakati Jordan inakabiliwa na changamoto zinazozidi kuongezeka za maji. Nchi hiyo, yenye takriban watu milioni 11.3, huagiza sehemu kubwa ya chakula chake kutoka nje, huku maji ya manispaa yakigawiwa kwa mgao. Katika baadhi ya maeneo, kaya hupata maji ya mabomba kwa saa 12 tu kwa wiki, na hutegemea matangi ya kuhifadhia maji juu ya paa ili kukidhi mahitaji yao.

3499739

captcha