IQNA

Mashindano ya Qur'ani

Mashindano ya Kimataifa ya Qur'ani ya wanawake Jordan yamalizika

14:51 - February 24, 2024
Habari ID: 3478408
IQNA - Toleo la 18 la mashindano ya kimataifa ya Qur'ani ya Jordan kwa wanawake yalihitimishwa katika hafla ambayo walioshika nafasi za juu walitangazwa na kutunukiwa.

Sherehe hiyo ilifanyika Alhamisi katika ukumbi wa mikutano wa Kituo cha Utamaduni cha Kiislamu kinachohusiana na Msikiti wa Mfalme Abdullah I huko Amman, tovuti ya Akhbar al-Hayat iliripoti.

Hafla hiyo imehutubiwa na Waziri wa Masuala ya Kiislamu na Wakfu Jordan Mohammad Ahmad Muslim Al Khalayleh, ambaye alisema mashindano hayo yameandaliwa kwa kuzingatia juhudi za nchi hiyo ya Kiarabu za kuwahudumia wanaharakati wa Qur'ani na Qur'ani.

Alisema wanawake na wasichana wote walioshiriki mashindano hayo ni washindi na watatunukiwa na Mwenyezi Mungu.

Waziri wa Wakfu ameongeza kuwa, kujifunza mafundisho ya Qur'ani, kanuni za kimaadili na fadhila za Kitabu hicho ndio mafanikio makuu ya wanaharakati wa Qur'ani.

Hajjar Ibrahim kutoka Nigeria alinyakua tuzo ya juu, Aisha Othman kutoka Chad alikuwa mshindi wa pili na zawadi ya tatu ilikwenda kwa Neda Abdul Basit kutoka Libya.

Nureddin Abdul Rahman kutoka Lebanon na Ahud bint Khamis kutoka Oman walishika nafasi ya nne na ya tano mtawalia.

Mashindano hayo ya kimataifa ya Qur'ani ya Jordan kwa wanawake, yanayojulikana kama "Al-Hashimiya", yalianza mjini Amman Jumamosi iliyopita kwa kushirikisha wahifadhi wa Qur'ani kutoka nchi 39.

 

 

captcha