Msikiti huo uko katika mtaa Tilal Al Ghaf , jijini Dubai ambapo una paneli 203 za sola zinazozalisha zaidi ya kWh 204,121 kila mwaka hiyo ikiwa ni asilimia 115 ya mahitaji yake ya nishati. Nishati ya ziada inarejeshwa kwenye gridi ya taifa.
Msikiti huo unajumuisha teknolojia nyingi zenye kuzingatia utunzaji mazingira kwa kupunguza matumizi ya umeme na maji, ikiwa ni pamoja na kupasha maji moto kwa nishati ya jua, taa za LED, vituo vya kuchaji magari ya umeme, na mfumo wa hali ya juu wa HVAC.
Pia ina Mfumo wa Usimamizi wa Jengo (BMS) ili kuboresha matumizi ya nishati. Shirika la Majid Al Futtaim ambalo limesimamia ujenzi wa mtaa huo linalenga kufikia uidhinishaji wa BREEAM kwa msikiti, kiwango kinachotambulika kimataifa katika ujenzi endelevu.
Ahmed Darwish Al Muhairi, meneja mkuu wa Idara ya Masuala ya Kiislamu na Shughuli za Hisani ya Dubai, aliashiria kuzinduliwa kwa msikiti huo kama hatua muhimu kwa malengo endelevu ya UAE, ikiwiana na msisitizo wa Dira ya UAE ya 2030 ya kusawazisha ukuaji wa uchumi na uhifadhi wa mazingira. Al Muhairi alielezea matumaini kuwa mradi huo utahamasisha mipango zaidi ya kijani kikanda na kimataifa.
Mkurugenzi Mtendaji wa Majid Al Futtaim, Ahmed Galal Ismail, alielezea msikiti huo kama heshima kwa maadili ya mwanzilishi wa kampuni na msingi wa jamii. "Msikiti huu ni ishara ya kujitolea kwa mwanzilishi wetu kutumikia jamii kwa mfumo endelevu wenye kutunza mazingira. Muundo wake unaonyesha maadili ya ufahamu wa mazingira katika Uislamu," alisema.
Msikiti huo uliojengwa kwa kutumia nyenzo zenye kaboni ya chini kwa kuzingatia utumizi bora wa maji hewa ya ndani, unatoa mfano wa muundo unaozingatia mazingira yanayolenga kudumisha mazingira yenye afya.
Mifumo ya mitambo, umeme, na mabomba ya msikiti huo ni muhimu kwa utendakazi wake chanya, ikisisitiza maono ya Majid Al Futtaim ya mustakabali safi na endelevu.
3490610