IQNA

Msomi: Mtume Muhammad (SAW) alihimiza kuhusu kutunza mazingira

17:20 - August 28, 2025
Habari ID: 3481149
IQNA – Mwanafunzi kutoka Chuo Kikuu cha Imam Sadiq (AS) nchini Iran ameelezea Sira na mafundisho ya Mtume Muhammad (S.A.W.) kuhusu ulinzi wa mazingira, ikiwemo yale yanayohusu kutotumia maji ovyo.

Akizungumza na IQNA, Hujjatul Islam Seyed Ali Hosseini alisema kuwa hata alipokuwa akifanya wudhuu karibu na mto unaotiririka, Mtume (SAW) alijali suala la kuokoa maji au kuzuia israfu ya maji. Mwenyezi Mungu anasema katika Qur’ani Tukufu, “Hakika, mna mfano mzuri katika Mtume wa Mwenyezi Mungu kwa yule anaye matumaini kwa Mungu na Siku ya Mwisho, na ambaye anamtaja Mungu sana,” alisema, akiongeza, “Kwa msingi huu, tunaweza kusema kuwa maisha ya Mtume Muhammad (SAW) yanaweza kuwa njia yetu ya maisha, na hii ni njia bora inayojenga dunia na wanadamu na kutupeleka kwenye furaha ya dunia na akhera.” 

Mtaalamu huyo alitaja kitabu kilichoitwa “Mazingira Asilia Katika Hadithi za Mtume" na kusema kwamba kitabu hicho kinabaini kuwa Mtume (SAW) alianzisha kanuni wazi na muhimu kuhusu maumbile asilia na mazingira. “Moja ya masuala muhimu ya mazingira ni maisha ya mimea na ulinzi wa kutosha wa majani duniani,” alisema mtaalamu huyo. “Mimea ya kijani kibichi ina thamani isiyokuwa na kifani. Bila ya mimea hii, dunia ingekuwa kama kaburi ambapo hakuna baraka wala uhai unaoonekana.” Mwanazuoni huyo alisisitiza kuhusu juhudi kubwa za Mtume (SAW) katika kupanda miti. “Mtume Muhammad (SAW) aliweka msisitizo mkubwa kwenye upandaji miti na kukuza mimea. Alitumia njia mbalimbali na mbinu kuwatia moyo Waislamu na kuwahamasisha ili kukuza ulinzi wa mimea.”

Mafundisho haya pia yalikwenda mbali hadi wakati wa vita, alibainisha, akielezea maagizo maalum ya vita. “Mtume (SAW) alikemea vikali kukata miti na alisisitiza mara kwa mara kwamba miti haitakiwi kukatwa, hata wakati wa vita.” Hujjatul Hosseini alirejelea kanuni za vita na kusema, “Tunajua kwamba katika vita, kanuni za kibinadamu zinazohusiana na maisha ya binadamu zinapuuziliwa mbali. Lakini Mtume (SAW) aliwaamuru Waislamu katika vita kutowaua wazee, watoto, wala wanawake. Alisema pia, ‘Msikate miti, msichome mashamba, msifanye mabonde ya mitende kuwa majangwa, na msisambaze sumu katika ardhi.’”

Alisisitiza pia mafundisho ya Mtume (SAW) kuhusu kuepuka matumizi mabaya ya maji. Hii ilihusiana hata na ibada kama vile wudhuu, alieleza mtaalamu, akirejelea hadithi kuhusu Mtume (SAW) na mmoja wa wafuasi wake, Sa’d. “Sa’d alianza kufanya wudhuu, na Mtume (S.A.W.) akamwambia: ‘Sa’d! Usitumie maji vibaya, hata kwenye kingo za mto unaotiririka. Huna haki ya kutumia maji  vibaya wakati wa kufanya wudhuu.’” Hujjatul Islam Hosseini alisema Hadithi kuhusu kuepuka uchafuzi na matumizi mabaya ya maji ni nyingi sana.

 Alibainisha uhusiano wa mafundisho haya na changamoto za kisasa na kusema. “Tatizo kuu la maji katika nchi yetu (Iran) sasa ni matumizi mabaya ya maji. Tunafungua bomba na kuacha maji yatiririke bila kutumiwa. Tunatumia maji vibaya katika kilimo, na njia kuu ya umwagiliaji kwa mashamba na bustani ni umwagiliaji wa mafuriko, ambayo husababisha matumizi mabaya ya maji.” Alieleza kwamba kufuata maelekezo ya Mtume (SAW) kunaweza kutatua matatizo ya sasa. “Ikiwa tutatumia maji tunayopata kwa njia aliyoagiza Mtume wa Mungu, tatizo letu la uhaba wa maji litapungua sana au kutoweka kabisa.”

3494398

captcha