IQNA

Oxfam yakosoa nchi tajiri kwa kuiuzia Saudia silaha zinazotumiwa kuwaua Wayemen

22:21 - November 18, 2020
Habari ID: 3473370
TEHRAN (IQNA) - Shirika la misaada ya kibinadamu la Oxfam lenye makao makuu yake nchini Uingereza limesema nchi 20 zenye uchumi mkubwa zaidi duniani (G20) zimeiuzia Saudi Arabia silaha zenye thamani ya dola bilioni 17 tangu Riyadh ianzishe vita dhidi ya Yemen mwaka 2015, lakini nchi hizo wanachama wa kundi la G20 zimeipa Yemen thuluthi moja ya fedha hizo kama msaada.

Katika ripoti yake ya jana Jumanne, Oxfam imesema inasikitisha kuona mauzo ya silaha zinazouzwa na nchi wanachama wa Kundi la G20 kwa Saudia, ni mara tatu ya msaada wa kibinadamu unaotolewa na mataifa hayo yaliyostawi kiuchumi kwa wananchi wa Yemen.

Ripoti hiyo ya shirika la misaada ya kibinadamu la Oxfam la Uingereza imetolewa kabla ya kuanza mkutano wa Kundi la G20 wiki hii nchini Saudi Arabia kwa njia ya intaneti.

Katika hali ambayo baadhi ya nchi za Ulaya zimesitisha mauzo ya silaha zao kwa utawala wa Aal-Saud, lakini aghalabu ya nchi za Kundi la G20 zingali zinaendelea kurundika silaha Saudia zinazotumika kuua raia wasio na hatia Yemen.

Oxfam inasisitiza kuwa, nchi mbalimbali zinapaswa kusimamisha uuzaji wa silaha kwa Saudi Arabia ili kuweza kukomesha mgogoro wa Yemen.

Nchi hiyo maskini ya Kiarabu inasumbuliwa na maafa makubwa zaidi ya kibinadamu duniani baada ya miaka kadhaa ya vita na mapigano.

Saudia ilianzisha mashambulizi dhidi ya Yemen mwishoni mwa mwezi Machi 2015 kwa lengo la kuiondoa madarakani Harakati ya Ansarullah na kumrejesha madarakani Abdrabbuh Mansour Hadi, rais wa zamani wa nchi hiyo aliyejiuzulu na kukimbilia Riyadh. Hata hivyo hadi sasa Saudia na washirika wake wameshindwa kufikia malengo yao kutokana na kusimama kidete wananchi wa Yemen. 

Mwezi Juni, Kituo cha Haki za Binadamu cha Ainul Insaniya kilitoa ripoti na kutangaza kuwa tokea muungano wa Saudia uanzishe vita dhidi ya Yemen mnamo Machi 26, 2015 hadi sasa watu 16, 672 wamepoteza maisha moja kwa moja kutokana na vita ambapo miongoni mwao kuna watoto 3,742 na wanawake 2,364.

3935892

 

Kishikizo: yemen watoto saudia oxfam
captcha