IQNA

Wasiwasi wa Al Azhar kuhusu pendekezo la Bunge la Misri la 'Tafsiri ya Kisasa' ya Qur'ani

16:13 - January 04, 2022
Habari ID: 3474764
TEHRAN (IQNA)- Wahadhiri wa Chuo Kikuu cha Al Azhar wamebainisha wasiwasi wao kuhusu pendekelezo la Bunge la Senate la Misri la kuandikwa 'Tafsiri ya Kisasa' ya Qur'ani.

Amna Nasser, mhadhiri wa itikadi na falsafa katika Chuo Kikuu cha Al Azhar amesema bado kuna haja ya kufanya utafiti zaidi kuhusu kadhia hii.

"Pendekezo hilo si sahihi kwani linaweza kuingiza dosari katika Qur'ani na kwa msingi huo suala hili halipaswi kushughulikiwa na watu wasio na weledi," amesema.

Mtamshi hayo  yamekuja baada ya Kamati ya Kidini katika Bunge la Misri limeanza kujadili pendekezo la kuandika tafsiri mpya ya Qur’ani Tukufu.

Yusuf Sayyid Amer, mwenyekiti wa kamati hiyo amewasilisha pendekezo  hilo ili lijadiliwe bungeni.

Ameongeza kuwa tafsiri mpya ya Qur’ani itakayotayarishwa itazingatia misimamo ya wastani katika Uislamu na kuwasilisha muelekeo wenye kukabiliana na misimamo mikali.

Halikadhalika amesema tafsiri hiyo italenga kujibu maswali kuhusu Hadithi ambazo makundi  yenye misimamo mikali hutumia katika kutetea misimamo yao mikali ya kidini, amesema Amer.

Pendekezo hilo limeibua gumzo na hisia mseto Misri.

Fathi Othman el Feqi, mhadhiri wa sheria amesema tafsiri yoyote ya Qur'ani inapaswa kutayarishwa wasomi na wataalamu waliobobea ili kuhakikisha kuwa ufahamu wa aya za Qur'ani haupotoshwei.

Aidha amesema tafsiri kama hiyo inapaswa kutayarishwa na Baraza la Maulamaa wa Al Azhar na taasisi husika huku akisisitiza kuwa neno 'kisasa' halipaswi kupelekea kutayarishwa tafsiri yenye kubadilisha au kupotosha aya za Qur'ani Tukufu.

Naye mchambuzi Qutb al-Arabi, amesema wasomi wasikae kimya kuhusu pendekezo hilo kwani limewasilishwa na wanasiasa na maafisa wa serikali ambao si wanazuoni au wataalamu katika masuala ya Qur'ani Tukufu.

4026042

captcha