IQNA

Nyota wa Liverpool, Mohammad Salah, akosolewa kutuma salamu za Krismasi

22:58 - December 26, 2021
Habari ID: 3474727
TEHRAN (IQNA)- Mcheza soka mahiri wa Misri Mohammad Salah ametuma ujumba wa salamu za Krismasi katika ukurasa wake wa Instagram akiwa na mke na watoto wake wawili.

Picha hiyo imeandamana na maandishi ya salaham za kheri na fanaka kwa Waksristo wakati huu wa  sherehe za Krismasi.

Fowadi huyo mwenye umri wa miaka 29, anayechezea timu ya Liverpool ya katika Ligi Kuu ya Uingereza, anajulikana kuwa mwenye kufungamana kikamilifu na mafundisho ya dini tukufu ya Kiislamu. Hatahivyo baadhi ya mashabiki wake Waislamu hawakufuriahia na wamemkosoa kwa kusherehehea Krismasi.

Hii si mara ya kwanza kwa Salah kutuma salamu za kheri na fanaka wakati wa Krismasi pamoja na kuwa yeye ni Muislamu.

Kuna hitilafu baina ya wanazuoni wa Kiislamu iwapo inafaa kwa Muislamu kutoa salamu za Krismasi.

Hatahivyo,  Dar al-Ifta ya Misri, anakotoka Salah, imesema inajuzu au ni sawa kwa Waislamu kuwapongeza wasiokuwa Waislamu kwa munasaba wa siku kuu zao na kwamba hilo ni kwa mujibu wa mafundisho ya dini tukufu ya Kiislamu.

Dar al-Ifta ya Misri, inayoshughulikia masuala ya fatuwa za Kiislamu, mwaka 2018 ilitangaza kuwa: "Mafundisho ya dini ya Kiislamu yanawahimiza Waislam kutoa salamu za pongezi kwa wasiokuwa Waislamu katika idi na minasaba yao ya kidini na hili ni kwa mujibu wa ubora wa tabia njema ambazo alikuja nazo Mtume SAW."

Katika ujumbe wake wa video, Dar al-Ifta ya Misri imetoa wito kwa Waislamu kufuatia Sira ya Mtume Muhammad SAW na kuwataka wasitumbukie katika mitego ya makundi ya wenye misimamo mikali ya kufurutu ada ambao wanawakufurisha wale wote wasioafiki fikra zao finyu.

Sheikhe Mkuu wa Al Azhar nchini Misri, ambayo ni taasisi kubwa zaidi ya kidini katika  Madhehebu ya Ahlu Sunna, pia hutuma salamu za Krismasi kwa viongozi wa Kikristo.

3477099

captcha