IQNA

Umuhimu wa kutafakari kuhusu matukio ya Karbala + Video

TEHRAN (IQNA)- Kufahamu historia na yaliyopita kunapaswa kumpelekea mwanadamu aweze kutafakari na kujitayarisha kwa ajili ya kujenga mustakabali mwema.

Hayo yamesemwa na Dkt. Muhsin Ismaili katika mfululizo wa mihadhara yake kuhusu mitazamo tafauti ya tukio la Ashura.

Akizungumza katika kikao chake cha nane, amesema kusoma, kusikiliza na kukumbuka yaliyojiri katika historia ya tukio la Ashura huko Karbala kunapaswa kupelekea mwanadamu aweze kutafakari kuhusu tukio hilo ili aweze kupata funzo na ibra kuhusu yaliyojiri.

Ameongeza kuwa Qur'ani Tukufu imetaja visa vya kaumu zilizopita na baada ya kutaja historia ya kaumu hizo mwanaadamu anatakiwa kutafakari na kupata funzo kutokana na yaliyopita.

Dkt. Ismaili anasema kwa msingi huo  kufahamu kuhusu yaliyopita kunapaswa kutongoza mtu katika kutadaburi  au kuzingatia na kutafakari ili tuweze kujenga mustakabali.

Amefafanua zaidi kuhusu nukta hiyo kwa kuashiria Aya  176 ya Sura Al-A'raaf katika Qur'ani Tukufu isemayo;  " Na tungelitaka tungeli mtukuza kwa hizo Ishara, lakini yeye aliushikilia ulimwengu na akafuata pumbao lake. Basi mfano wake ni mfano wa mbwa. Ukimhujumu hupumua na kutoa ulimi na ukimwacha pia hupumua na kutoa ulimi. Huo ni mfano wa kaumu wanao zikanusha Ishara zetu. Basi simulia hadithi, huenda wakatafakari."

Dkt. Ismaili amesema wakati tunapochunguza tukio la Karbala tunapaswa kutambua maadui wa zama hizi ambao wanashabihiana na maadui wa zama hizo kama vile Shimr ambaye ndiye aliyekuwa kamanda wa jeshi la Yazid ambalo lilimuua shahidi Imam Hussein AS na wafuasi wake 72 katika siku ya Ashura. Kwa msingi huo tukio la Karbala litabakia kuwa chuo cha kumfunza mwanadamu katika zama zote.

Katika mwezi wa Muharram Waislamu, hasa wa madhehebu ya Shia, na wapenda haki kote duniani hukumbuka  tukio la Ashura ambalo lilijiri takribani miaka 1382 iliyopita kulingana na kalenda ya Hijria Qamaria.

Katika tukio hilo, moja kati ya vita mashuhuri katika historia ya Kiislamu na ya mwanadamu, vilitokea baina ya majeshi ya haki na batili katika ardhi ya Karbala huko Iraq. Siku hii inajulikana kwa jina la Ashura. Katika siku hiyo mjukuu wa Mtume SAW, Imam Hussein bin Ali bin Abi Twalib AS, alisimama kishujaa na wafuasi wake waaminifu 72, kukabiliana na jeshi la batili ili kuilinda dini ya Allah. Hamasa ya Karbala ilikuwa dhihirisho la mambo mawili makuu. Kwanza ni ujasiri, ushujaa, moyo wa kujitolea, uaminifu pamoja na kuyapokea kwa moyo mkunjufu mauti ya kuuawa shahidi, sifa walizojipamba nazo wapiganaji wachache wa jeshi la haki wakiongozwa na Imam Hussein AS dhidi ya Yazid bin Muawiya.

3475523

Kishikizo: ashura ، imam hussein as ، karbala ، ismaili