Idara ya Dar al-Qur’an ya Haram ya Imam Hussein (AS) ndiyo iliyoandaa maonesho haya, yaliyozinduliwa rasmi Jumatatu, Julai 14. Maonesho yataendelea kwa muda wa siku tatu.
Maonesho haya yanaonesha kazi zaidi ya 100 za kaligrafia kutoka kwa wasanii zaidi ya 35. Yameandaliwa na Kituo cha Kaligrafia ya Kiarabu na Kalamu, ambacho ni tawi la Dar al-Qur’an linalofungamana na Haram ya Imam Hussein (AS).
"Maonesho haya yamezinduliwa katika moja ya sehemu takatifu zaidi duniani, kati ya makaburi mawili matukufu," alisema Wisam al-Delfi, mkuu wa Kituo cha Habari za Qur’ani katika haram hiyo. "Yanaleta muunganiko wa kiroho na kisanii na Imam Hussein (AS) kupitia sanaa ya kaligrafia ya Kiarabu," aliongeza, akinukuliwa na idara ya habari ya eneo hilo takatifu.
Sherehe ya ufunguzi ilihusisha usomaji wa Qur’an uliotolewa na Ali Mousa, pamoja na hotuba kutoka kwa Sheikh Khayr al-Din Hadi, mkurugenzi wa Dar al-Qur’an, ambaye alisisitiza nafasi ya sanaa katika kuhifadhi kumbukumbu za kidini.
"Ni lazima tueleze mapenzi yetu kwa Imam Hussein (AS) kupitia sanaa za Kiislamu," alisema Sheikh Hadi. "Kitu chochote kinachohusiana na Imam Hussein (AS) kitaendelea kudumu milele."
Imam Hussein (AS), mjukuu wa Mtume Muhammad (SAW), aliuawa shahidi katika vita vya Karbala mwaka 61 Hijiria sawa na 680 Miladia baada ya kukataa kula kiapo cha utiifu kwa khalifa dhalimu wa Bani Umayyah, Yazid bin Muawiya. Kifo chake huwa kinaadhimishwa kila mwaka na mamilioni ya Waislamu wa Kishia duniani.
Kwa sasa, Karbala inajiandaa kuwapokea mamilioni ya wafanyaziara kutoka sehemu mbalimbali duniani kwa ajili ya ziara ya Arbaeen, mojawapo ya mikusanyiko mikubwa ya kidini duniani.
/3493846