Imam Hussein AS aliuawa shahidi kikatili mwaka wa 61 Hijria katika jangwa la Karbala nchini Iraq akiwa na umri wa miaka 57 baada ya kuongoza mapambano ya kishujaa ya ushindi wa damu mbele ya upanga.
Mtume Muhammad SAW alitabiriwa na Malaika Jibril ukatili huo aliofanyiwa mjukuu wake katika jangwa la Karbala, tangu enzi za uhai wake na alikuwa wa kwanza kumlilia mjukuu wake huyo kipenzi baada ya kuletewa mchanga na Malaika Jibril, wa eneo ambako Imam Hussein AS angeliuliwa shahidi.
Kwa kufuata sira na mwenendo huo wa Bwana Mtume Muhammad SAW, wafuasi wa Ahlul Bayt wa Mtume na wapenzi wa haki na wanaopiga vita dhulma, hadi leo hii na katika kila kona ya dunia, wanaendelea kukumbuka kwa huzuni na majonzi jinai hiyo kubwa waliyofanyiwa watu wa Nyumba tukufu ya Bwana Mtume Muhammad SAW na kumbukumbu hizo hufika kileleni leo mwezi kumi Muharram, kila mwaka.
Miongoni mwa matamshi ya Imam Husain AS kwenye jangwa la Karbala ambayo yamekuwa nembo na kigezo hadi leo hii ni pale aliposema: "Kama dini ya babu yangu (Uislamu) haitosimama ila kwa kuuliwa mimi, basi enyi panga chukueni roho yangu!"
Mamilioni ya Waislamu na hata wasiokuwa Waislamu wamejitokeza huko Karbala nchini Iraq, katika miji yote ya Iran na pia maeneo mengine duniani katika kumbukumbu ya kuuawa Shahidi Imam Hussein (AS).
4292848