IQNA

Mradi wa Tafsiri wa Al-Azhar Walenga Kusambaza Ujumbe wa Qur’ani Tukufu

10:48 - January 13, 2026
Habari ID: 3481798
IQNA – Kitivo cha Lugha cha Chuo Kikuu cha Al-Azhar nchini Misri kinaendeleza mradi mahsusi wa tafsiri na tarjuma unaolenga kuufikisha ujumbe wa Qur’ani Tukufu kwa mataifa mbalimbali duniani.

Mradi huo, unaojulikana kama “Tarjuma ya Vitabu 1,000”, unahusisha uteuzi na uhawilishaji wa kazi bora za kielimu na kifasihi za Al-Azhar kutoka Kiarabu kwenda lugha nyingine nyingi.

Kwa mujibu wa Profesa Khaled Abbas, mkuu wa kitivo hicho, mpango huu ni jukumu la kitaifa la kuufikisha ulimwenguni ujumbe wa Qur’ani na misingi ya Uislamu kwa lugha zinazofahamika na watu wa tamaduni tofauti.

Amesema kuwa Al-Azhar imebarikiwa kuwa na wanazuoni mahiri na wataalamu wa fani mbalimbali, kuanzia sayansi za Kiislamu, fasihi, falsafa hadi taaluma nyingine za juu, lakini bado watu wengi duniani hawajui ukubwa wa hazina ya machapisho ya chuo hicho. Ndiyo maana mradi huu umeanzishwa ili kuyawasilisha maarifa hayo kwa walimwengu kwa lugha wanazozimudu.

Al-Azhar Translation Project Aims to Spread Quran’s Message

Kwa ajili hiyo, kamati maalumu ikijumuisha rais wa Al-Azhar na wakuu wa vitivo mbalimbali iliundwa kuchagua kazi zitakazotafsiriwa.

Abbas ameongeza kuwa chuo hicho kina mpango wa kuanzisha kituo cha uchapishaji kitakachoshughulikia uchapishaji wa vitabu hivyo vilivyotafsiriwa katika siku zijazo.

Ushirikiano tayari umeanzishwa kati ya chuo hicho, Kituo cha Tafsiri cha Al-Azhar, na pia Dar al-Ifta ya Misri, ambayo ndiyo njia ya mawasiliano na zaidi ya vituo 200 vya kimataifa. Amesema nakala za PDF za vitabu vilivyotarjumiwa hutumwa bila malipo kwa vituo hivyo vya nje.

Soma zaidi:

Mkuu huyo wa kitivo cha lugha pia ametaja shughuli za idara za Kiingereza, Kijerumani, Kifaransa, Kichina na Kihispania, pamoja na idara ya masomo ya Kiislamu inayotoa masomo kwa Kiingereza, Kifaransa, Kiurdu na Kichina.

Aidha, kitivo hicho kimeshirikiana na Kituo cha Tafsiri cha Al-Azhar katika kutafsiri na kutarjumu Qur’ani Tukufu kwa lugha ya Kijerumani na Kihispania, miongoni mwa lugha nyingine.

Kuhusu mjadala unaoendelea duniani kuhusu iwapo akili bandia inaweza kuchukua nafasi ya watafsiri, Abbas amesema kwamba huenda siku zijazo mikutano na makongamano yasihitaji wakalimani wa papo kwa papo, lakini nafasi ya mtafsiri wa maandishi—hasa maandishi ya kidini, kisheria na kifasihi—itasalia kuwa ya lazima na isiyoweza kubadilishwa.

4323476

captcha