Mkutano huu uliofanyika Januari 20 uiandaliwa na Jumuiya ya Kimataifa ya Umoja na Kukurubisha Madhehebu ya Kiislamu (WFPIST) kwa ushirikiano na Baraza la Mashauriano la Mashirika ya Kiislamu Malaysia (MAPIM) pamoja na taasisi mbalimbali zinazounga mkono haki ya Palestina, na kwa kuhudhuriwa na wanazuoni, wasomi na wanafikra wa Kiislamu kutoka nchi za ASEAN.
Kwa mujibu wa taarifa ya kitengo cha mahusiano ya umma cha Jumuiya ya Kimataifa ya Kukurubisha Madhehebu ya Kiislamu, yafuatayo ni dondoo kutoka katika tamko la mwisho la mkutano:
Kwa Jina la Allah Mwingi wa Rehema Mwenye Kurehemu
Sisi, wanazuoni wa dini, wasomi, viongozi wa kidini na wawakilishi wa taasisi za Kiislamu kutoka sehemu mbalimbali za ulimwengu wa Kiislamu, tuliokusanyika katika Mkutano wa Umoja wa Ummah wa Kiislamu kwa Ajili ya Palestina, uliofanyika Kuala Lumpur, Malaysia, Januari 20, 2026, kwa mwaliko wa Serikali ya Malaysia na kwa ushirikiano na Jumuiya ya Kimataifa ya Kukurubisha Madhehebu ya Kiislamu, tunatoa Tamko hili la Kuala Lumpur.
Mkutano huu umefanyika katika kipindi cha kihistoria na chenye uzito mkubwa, wakati ambapo jinai zisizowahi kushuhudiwa zinatendwa na utawala wa Kizayuni unaonyakua ardhi, dhidi ya watu wa Palestina, hasa katika Ukanda wa Gaza. Miongoni mwa ukatili huo ni mauaji ya halaiki, kuuawa kwa makumi ya maelfu ya raia wasiokuwa na hatia, waliowengi wakiwa wanawake na Watoto,kujeruhiwa kwa mamia ya maelfu, uharibifu mkubwa wa nyumba na miundombinu, pamoja na kung’olewa makwao kwa zaidi ya watu milioni mbili. Matendo haya, kwa mujibu wa vigezo vya kimataifa, yanaingia katika dhana ya mauaji ya kimbari na uhalifu dhidi ya ubinadamu.
Baada ya kuchambua kwa kina mwelekeo wa matukio ya kikanda na kimataifa, na tukihisi wajibu wetu wa kidini, kimaadili na kihistoria, tunatangaza mshikamano wetu wa dhati na watu wa Palestina wanaodhulumiwa. Tunawapa salamu za heshima mashahidi wa Gaza, na tunatangaza yafuatayo:
1. Umoja wa Ummah wa Kiislamu
Ummah wa Kiislamu ni ummah mmoja: unamwabudu Mungu Mmoja, unamfuata Mtume mmoja, unasoma Kitabu kimoja, na unakielekea Kibla kimoja.
2. Heshima ya Mwanadamu, Uadilifu na Kusimama dhidi ya Dhulma
Heshima ya mwanadamu, uadilifu na usalama ni nguzo kuu za maadili ya Kiislamu. Heshima ya binadamu ni neema ya Mwenyezi Mungu kwa kila mtu, na uadilifu ni amri ya Kiungu na ya kiakili inayotoa msingi wa uhalali wa utawala na utulivu wa jamii. Kukiukwa kwa haki za binadamu ni aina ya dhulma inayopaswa kukataliwa na kupingwa kwa kauli moja.
3. Ushirikiano wa Kiislamu kama Msingi wa Umoja
Kupatikana kwa umoja wa Waislamu kunahitaji kuimarishwa kwa ushirikiano wa Kiislamu kati ya madhehebu, mataifa na taasisi. Tofauti zilizopo ndani ya Ummah ni chanzo cha utajiri wa fikra na uzoefu, si sababu ya mgawanyiko. Ushirikiano unaojengwa juu ya mambo ya pamoja ndio msingi wa kujenga mustakabali uliojaa udugu na maelewano.
4. Kukataa Uchochezi wa Kimadhehebu
Tunatoa onyo kuhusu hatari ya uchochezi wa kimadhehebu na hotuba za kuchochea chuki ambazo hudhoofisha Ummah na kuwanufaisha maadui wake. Kutukana Waislamu au kushambulia alama na nembo za dini kunazaa uhasama na kuporomoka kwa maadili.
5. Palestina na Al-Quds kama Agenda ya Pamoja
Kadhia ya Palestina, Al-Quds na Ardhi Takatifu ni suala la msingi na la pamoja kwa Ummah wa Kiislamu. Kuunga mkono watu wa Palestina wanaodhulumiwa ni jukumu la kidini na kimaadili, na ni sehemu ya wajibu wa kulinda haki na uadilifu katika ardhi ya Kiislamu.
6. Msaada kwa Upinzani na Uwajibikaji
Tunatangaza kuunga mkono safu ya Muqawama (mapambano) dhidi ya utawala wa Kizayuni unaotenda jinai, na tunataka wahusika wa uhalifu wa kivita wawajibishwe. Tunasisitiza pia juu ya kuachiliwa mara moja na bila masharti kwa wafungwa wa Kipalestina, pamoja na kuungwa mkono kwa uchunguzi huru wa kimataifa.
7. Hatua za Kivitendo na Vikwazo
Tunatoa wito wa kusitishwa mara moja kwa mashambulizi dhidi ya Gaza na kuondolewa kwa mzingiro. Tunataka kukatwa kwa mahusiano ya kisiasa, kiuchumi na kidiplomasia na utawala wa Kizayuni wa Israel, kuwekwa kwa vikwazo vya kina, kususiwa kabisa kwa bidhaa zake, na kutolewa kwa msaada wa kibinadamu, kifedha na wa kiulinzi kwa watu wa Palestina.
Mwisho wa Mkutano
Mwishoni mwa mkutano huu, tunawakumbuka kwa heshima mashahidi wa Muqawama, tunapongeza ujasiri na ustahamilivu wa watu wa Palestina, na tunatoa wito kwa serikali za Kiislamu, wanazuoni wa dini, jamii za kiraia, na watu wote huru duniani kuchukua hatua madhubuti ili kurejesha haki halali na kamili za watu wa Palestina.