IQNA

Mkutano wa Morocco Kujadili “Tafsiri ya Qur’ani na Akili Mnemba (AI)”

10:14 - January 25, 2026
Habari ID: 3481845
IQNA – Toleo la pili la mkutano wa kimataifa kuhusu “Tafsiri ya Qur’ani na Akili Mnemba” linatarajiwa kufanyika nchini Morocco.

Tukio hili la kisayansi linaandaliwa na Kituo cha Ibn Al-Jazari cha Tafiti na Utafiti kwa ushirikiano na taasisi mbalimbali za kitaifa na kimataifa za kielimu, kitaaluma na kijamii, kwa mujibu wa taarifa za ammonnews. Kwa kaulimbiu “Tafsiri ya Qur’ani na Akili Mnemba: Kuelekea Mtazamo wa Kimetodolojia na Wajibu wa Kuelekeza”, mkutano utafanyika tarehe 18 na 19 Julai 2026. Kongamano hili linawekwa katika muktadha mpya wa fikra unaotambua nafasi ya Qur’ani Tukufu kama chanzo kikuu cha mwongozo na sheria kwa Ummah wa Kiislamu, huku likijishughulisha kwa makini na mabadiliko ya zama za akili mnemba. Lengo lake ni kuchunguza uwezo wa teknolojia za kisasa za kidijitali katika kuhudumia tafsiri ya Qur’ani ndani ya mfumo wa kisayansi na kimaadili unaolinda utukufu wa maandiko ya Qur’ani na kuzingatia misingi yake ya msingi.

Mkutano wa Meknes unalenga kuendeleza mtazamo sahihi wa kimetodolojia wa kile kinachoitwa “tafsiri mahiri”, unaochanganya urithi wa tafsiri za jadi na uwezo wa akili mnemba. Pamoja na kuunda mtandao wa kimataifa wa utafiti unaounganisha vyuo vikuu na vituo maalumu vya kisayansi, juhudi hizi pia zinakusudia kuandaa hati ya kimataifa ya maadili ya matumizi ya akili mnemba katika masomo ya Qur’ani. Ratiba ya kisayansi ya mkutano inajumuisha mada muhimu kama misingi ya kifikra ya tafsiri mahiri, uchakataji wa lugha asilia kwa maandiko ya Qur’ani, uchambuzi wa miundo ya majukwaa ya tafsiri mahiri, pamoja na miongozo ya kisheria na kimaadili kuhusu matumizi ya algoriti katika kutafsiri maandiko ya kidini.

Siku ya pili itatengwa kwa warsha za vitendo zitakazoendeshwa na wataalamu wa tafsiri na akili bandia, kwa manufaa ya wanafunzi, watafiti na wadau, ili kuyageuza matokeo ya mkutano kutoka nadharia kwenda matumizi ya moja kwa moja.

Habari inayohusiana

Kamati ya maandalizi imeweka tarehe 28 Februari 2026 kuwa mwisho wa kutuma muhtasari wa tafiti kupitia barua pepe centrejazari19@gmail.com, huku tarehe ya mwisho ya kuwasilisha tafiti kamili ikiwa 30 Mei 2026. Tukio hili la kielimu linatarajiwa kuwaleta pamoja maprofesa, watafiti, wanafunzi wa uzamili, wapangaji programu, taasisi na vituo vinavyovutiwa na masomo ya Qur’ani na teknolojia.

Inafaa kuashiria hapa kuwa Akili Mnemba au Akili Unde na pia Akili Bandia (kwa Kiingereza: Artificial Intelligence, kifupi: AI) ni nadharia ya uundaji wa mifumo ya kompyuta yenye uwezo wa kutekeleza kazi ambazo kwa kawaida zinahitaji akili ya binadamu, kama kuona, kutambua sauti, kufanya maamuzi au kutafsiri lugha. Lengo lake si tu kufanya kazi kwa kasi, bali pia kufanya kazi kwa busara, kulingana na mazingira na taarifa mpya.

4330036

Habari zinazohusiana
Kishikizo: akili qurani tukufu
captcha