IQNA

Wang Yi: China iko tayari kushirikiana na nchi za Kiislamu kulinda haki

14:41 - January 27, 2026
Habari ID: 3481857
IQNA – Waziri wa Mambo ya Nje wa China, Wang Yi, amefanya mazungumzo na Hissein Brahim Taha, Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu (OIC), mjini Beijing siku ya Jumatatu.

Katika taarifa rasmi ya Wizara ya Mambo ya Nje ya China, Wang alisema kuwa Beijing iko tayari kushirikiana na nchi za Kiislamu kulinda “haki na maslahi halali” ya mataifa yanayoendelea na kupinga kurejea kwa dunia katika “sheria ya msituni”. Alisisitiza kuwa pande zote mbili zinapaswa kuzingatia ushirikiano wa kiwango cha juu ndani ya Mpango wa Ukanda na Njia (Belt and Road Initiative), kuendeleza suluhu za kisiasa kwa migogoro ya kikanda, na kulinda amani na uthabiti katika Asia Magharibi (Mashariki ya Kati).

Wang aliongeza kuwa Beijing imekuwa ikipa kipaumbele cha kimkakati kuendeleza uhusiano na nchi za Kiislamu pamoja na OIC, na inathamini msimamo wao thabiti kuhusu suala la Taiwan. Aidha, aliitaka pande zote mbili kuendeleza “ushirikiano wa kweli wa kimataifa”, kulinda nafasi ya Umoja wa Mataifa kama mhimili wa mfumo wa kimataifa, na kuchangia katika kujenga utawala wa dunia ulio wa haki na usawa zaidi.

OIC, ikiwa shirika kubwa zaidi la kiserikali katika ulimwengu wa Kiislamu, ni “alama muhimu ya umoja na uhuru wa nchi za Kiislamu,” alisema Wang.

Kwa upande wake, Taha alisema kuwa OIC “inapinga kuingiliwa kwa masuala ya ndani ya China,” na “iko tayari kushirikiana na China kuimarisha ushirikiano wao na kwa pamoja kulinda amani, uthabiti na ustawi wa kikanda.” Alisifu pia “mchango mkubwa wa China katika kutafuta suluhu ya kina, ya kudumu na ya haki kwa suala la Palestina,” na akatarajia China itaendelea kuchukua nafasi kubwa zaidi katika juhudi hizo.

Habari inayohusiana:

Makamu wa Rais wa China, Han Zheng, pia alikutana na Taha, akibainisha kuwa OIC ni daraja muhimu katika kuimarisha uhusiano wa China na nchi za Kiislamu.

3496203

Kishikizo: china oic
captcha