
Mamlaka hiyo imeonya kuwa kutegemea zana kama hizi kunaweza kusababisha upotoshaji wa maana na kusambaa kwa taarifa zisizo sahihi.
Hukumu hiyo imetolewa kufuatia swali lililotaka ufafanuzi kuhusu iwapo zana za akili mnemba zinaweza kutumiwa katika kutafsiri aya za Qur’ani.
Dar al‑Ifta ilibainisha kuwa kutegemea kikamilifu au kwa kujitegemea tafsiri zinazozalishwa na akili mnemba ni jambo lililokatazwa katika Uislamu, kwa kuwa kunaiweka Qur’ani katika hatari ya kubebeshwa dhana, makosa na upotoshaji.
Mamlaka hiyo ilisisitiza kwamba uelewa sahihi wa Qur’ani lazima ujengwe juu ya vitabu vinavyotambuliwa vya Tafsiri pamoja na mwongozo wa wanazuoni waaminifu na taasisi madhubuti za kidini.
Ilionya kuwa kuacha vyanzo sahihi kunaweza kusababisha mkanganyiko, makosa ya kiitikadi na kusambaa kwa maelezo yasiyo na uthibitisho.
Kwa mujibu wa hukumu hiyo, teknolojia za akili mnemba hufanya kazi kwa kuchakata data kiotomatiki na kutumia mifumo ya takwimu, bila uwezo wa kuelewa kwa hakika maandiko ya Qur’ani. Hivyo, matokeo yake yanaweza kuwa na makosa ya kiuhalisia, taarifa zisizothibitishwa au yaliyomo yanayokwenda kinyume na mafundisho ya Kiislamu.
Habari inayohusiana:
Dar al‑Ifta ilitaja hatari kadhaa zinazohusiana na tafsiri za Qur’ani zinazotegemea akili mnemba, ikiwemo kutokuwa na uhakika wa vyanzo, kushindwa kuthibitisha usahihi, na kukosekana kwa mbinu madhubuti za kielimu. Upungufu kama huo, ilionya, unaweza kusababisha Qur’ani kupewa maana zisizo sahihi.
Mamlaka hiyo ilikumbusha kwamba Waislamu wanaotaka kuelewa Qur’ani wanapaswa kurejea kazi za tafsiri zilizo sahihi, wanazuoni waliobobea na taasisi za dini zenye kuaminika ili kupata ufafanuzi ulio sahihi na wa kutegemewa.
3496212