IQNA

Ongezeko kubwa la ujenzi wa Misikiti Kazakhstan

11:01 - January 28, 2026
Habari ID: 3481860
IQNA – Idadi ya misikiti mipya inayofunguliwa nchini Kazakhstan imekuwa ikiongezeka kwa kasi katika miaka ya karibuni, ishara ya mwamko wa Kiislamu unaoendelea kushika mizizi katika taifa hilo la Asia ya Kati.

Mwaka 2025 pekee, misikiti 20 mipya ilizinduliwa kote nchini, ongezeko la asilimia 54 ikilinganishwa na mwaka uliotangulia. Huu ndio ukuaji wa juu zaidi kuwahi kurekodiwa katika kipindi cha muongo mmoja, kwa mujibu wa taarifa za idara ya takwimu inayojulikana kama First Credit Bureau (FCB).

Takwimu za kihistoria zinaonyesha mwelekeo thabiti wa kuongezeka kwa ujenzi wa miundombinu ya kidini. Kati ya mwaka 2021 na 2025, wastani wa misikiti mipya ulifikia 17.4 kwa mwaka, karibu mara mbili ya wastani wa 8.8 ulioshuhudiwa katika kipindi cha miaka mitano kilichotangulia.

FCB ilibainisha kuwa ni vigumu kulinganisha moja kwa moja misikiti iliyojengwa katika miaka tofauti kutokana na ukosefu wa takwimu za wazi kuhusu uwezo wake wa kuhudumia waumini. Hata hivyo, taarifa zinazopatikana kuhusu gharama halisi za ujenzi zinatoa mwanga wa kulinganisha kwa njia isiyo ya moja kwa moja.

Kwa mujibu wa Bureau hiyo, ufadhili wa ujenzi mwaka 2025 uliongezeka karibu mara tatu ukilinganishwa na mwaka uliopita, na kufikia jumla ya tenge bilioni 12.6. Ingawa ni kiwango kikubwa, si rekodi ya juu kabisa. Kwa mfano, mwaka 2022 ufadhili ulipanda hadi tenge bilioni 118.8, ambapo asilimia 97 ya fedha hizo (tenge bilioni 114.9) zilielekezwa jijini Astana kwa ajili ya kukamilisha Msikiti Mkuu wa jiji hilo—msikiti mkubwa zaidi katika Asia ya Kati.

Habari inayohusiana:

Kwa sasa, eneo la Kyzylorda linaongoza kitaifa kwa idadi ya misikiti mipya na kiwango cha matumizi, likiwa na misikiti 11 yenye thamani ya tenge bilioni 9.7. Eneo hilo limekuwa kinara kwa miaka miwili mfululizo, tofauti kabisa na hali kabla ya 2021 ambapo ujenzi wa misikiti ulikuwa karibu kutokuwepo.

Mbali na Kyzylorda, misikiti mipya pia ilikabidhiwa katika maeneo manne mengine mwaka 2025: Kazakhstan ya Magharibi, Aktobe, Zhambyl na Akmola.

3496214

Kishikizo: kazakhstan misikiti
captcha