IQNA

Maulamaa Waislamu duniani waharamisha uhusiano na Israel

19:53 - November 28, 2021
Habari ID: 3474612
TEHRAN (IQNA)- Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Kimataifa ya Wanazuoni wa Kiislamu (IUMS) amelaani hatua ya baadhi ya nchi za Kiarabu ya kuanzisha uhusiano na muungano na utawala haramu wa Kizayuni wa Israel na kusaini mikataba ya mapatano na utawala huo ghasibu.

Katika taarifa, Sheikh Dkt. Ali Mohyiddeen Al-Qaradaghi katibu mkuu wa Jumuiya ya Kimataifa ya Wanazuoni wa Kiislamu amesema nchi kama vile Umoja wa Falme za Kiarabu na Morocco zimefanya kitendo haramu kwa kuanzisha uhusiano na utawala wa Kizayuni wa Israel na kusema hatua kama hivyo ni usaliti dhidi ya taifa la Palestina.

Aidha ametilia mkazo msimamo wa jumuiya hiyo wa kuunga mkono Msikiti mtukufu wa Al Aqsa na Palestina na kulaani hatua ya kuanzisha uhusiano wa kawaida na utawala haramu wa Kizayuni itakayochukuliwa na nchi yoyote au kundi lolote lile.

Umoja huo vilevile umetaka zifanyike kila jitihada za uungaji mkono wa kifedha na kimaanawi kwa ajili ya kuzikomboa ardhi zote zinazokaliwa kwa mabavu na utawala wa Israel hasa msikiti wa Al Aqsa na Quds tukufu (Jerusalem).

Sheikh al-Qaradaghi  amesema mwenyekiti wa Jumuiya ya Kimataifa ya Wanazuoni wa Kiislamu Sheikh Ahmed al Raissouni, ambaye ni raia wa Morocco, naye pia amelaani hatua ya Morocco kuanzisha uhusiano na utawala wa Kizayuni wa Israel na ameandika makala maalumu kuhusu hatari ya kitendo hicho.

Nchi nne za Kiarabu za Imarati (UAE), Bahrain, Morocco na Sudan mwaka uliopita wa 2020 zilisaini hati za makubaliano ya kuanzisha uhusiano wa kawaida na utawala haramu wa Kizayuni wa Israel, hatua ambayo imepingwa na kulaaniwa vikali katika nchi za Kiarabu na Kiislamu.

4016672

captcha