IQNA

Walowezi wa Kizayuni waendeleza hujuma dhidi ya msikiti mtakatifu wa al-Aqsa

19:45 - January 11, 2022
Habari ID: 3474794
TEHRAN (IQNA) - Makumi ya walowezi wa Kizayuni wameuvamia tena msikiti wa al-Aqsa katika mji wa Quds (Jerusalem) ambapo wameuvunjia heshima msikiti huo ambao ni kibla cha kwanza cha Waislamu.

Ripoti ya Palestina al-Yaum inaeleza kuwa, katika muendelezo wa hujuma na vitendo vya chuki vya utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya wananchi wa Palestina, makumi ya walowezi wa Kiyahudi jana walivamia tena msikiti mtakatifu wa al-Aqsa.

Walowezi hao wa Kizayuni wakisaidiwa na kupewa himaya na jeshi la Israel baada ya kuingia katika eneo la ndani la msikiti huo mtakatifu walisikika wakipiga nara dhidi ya Uislamu na Waislamu.

Wazayuni hao walivamia eneo hilo takatifu kupitia upande wa Babul-Magharibah na kuanza kufanya vitendo vya kichochezi.

Katika miaka ya hivi karibuni, utawala wa Kizayuni wa Israel umeshadidisha hujuma na uvamizi wake dhidi ya maeneo ya Wapalestina ukifanya njama za kufikia malengo yake haramu katika ardhi za Wapalestina.

Msikiti wa al-Aqsa ambao ni kibla cha kwanza cha Waislamu umekuwa ukiandamwa na njama mtawalia za utawala vamizi wa Israel, hatua ambazo zinakwenda sambamba na ujenzi wa vitongoji vya walowezi wa Kizayuni katika maeneo ya Wapalestina.

4027863

captcha