IQNA

Mtazamo wa Qur'ani
19:18 - May 27, 2022
Habari ID: 3475303
TEHRAN (IQNA)- Katibu Mkuu wa Umoja wa Wanazuoni wa Kiislamu Duniani amelaani mauaji ya kiholela hivi karibuni katika shule huko Texas, Marekani ambapo watu 22 waliuawa huku akiashiria aya ya 32 ya Sura Al Maidah katika Qur'ani Tukufu inayozungumzia matukio kama hayo ya mauaji yasiyo na msingi.

Katika taarifa ambayo imesambazwa kwa vyombo vya habari ikiwemo IQNA, Sheikh Dkt. Ali Mohyiddeen Al-Qaradaghi Katibu Mkuu wa Umoja wa Wanazuoni wa Kiislamu Duniani ameonya kuhusu hatari ya chuki, ubaguzi wa rangi, kuporomoka maadili na itikadi kali, yote ambayo ni tishio kwa jamii ya mwanadamu.

Katika taarifa hiyo, Umoja wa Wanazuoni wa Kiislamu Duniani umelaani jinai mbaya ya ufyatuaji risasi katika shule ya msingi katika jimbo la Texas nchini Marekani ambapo idadi kubwa ya watoto wasio na hatia wameuawa.

Sheikh Ali Qaradaghi, ameashiria sehemu ya Aya ya 32 ya Sura Al-Maidah katika Qur'ani Tukufu inayosema: "...Aliye muuwa mtu bila ya yeye kuuwa, au kufanya uchafuzi katika nchi, basi ni kama amewauwa watu wote..."

Amesema huu ndio msimamo thabiti wa Umoja wa Wanazuoni wa Kiislamu Duniani katika kukataa vurugu, utumiaji mabavu na vitendo vya uhalifu.

Sheikh Ali Qaradaghi ameendelea kusema kuwa,  jinai kama ile iliyotendeka Texas haiwezi kutetewa hata kidogo na ni haramu kwa mujibu wa dini.

Hatimaye Umoja wa Wanazuoni wa Kiislamu Ulimwenguni umezitaka serikali na asasi husika za kiraia kote duniani kuingilia kati mara moja na kuchukua hatua zinazohitajika kwa kuimarisha imani kwa Mwenyezi Mungu, maadili mema, upendo baina ya watu, kukabiliana na chuki na ubaguzi wa rangi na kutunga sheria zenye uwezo wa kuzuia kutendeka kwa uhalifu huu.

Siku ya Jumanne ufyatuaji risasi kiholela uliotokea katika shule moja huko Uvalde, Texas nchini Marekani. Waliofariki katika ufyatuaji risasi huo ni watu 22, 19 kati yao wakiwa ni watoto wadogo na wengine watatu watu wazima. Mshambuliaji alikuwa mvulana wa miaka 18 anayeitwa Salvador Ramos ambaye pia aliuawa.

Mauaji yanayotokana na matumizi mabaya ya silaha, na ambayo ni mojawapo ya matatizo sugu zaidi nchini Marekani yanaendelea kuongezeka siku baada ya nyingine na sasa yametoka kabisa katika udhibiti wa serikali na polisi ya Marekani.

4059966

Kishikizo: Marekani ، risasi ، texas ، Qaradaghi ، Kiislamu ، Al Maidah
Jina:
Baruapepe:
* maoni:
* captcha: