IQNA

Rais Aliyechaguliwa ni Rais wa Jamhuri na Taifa Zima la Iran

8:24 - June 14, 2009
Habari ID: 1790516
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Sayyed Ali Khamenei ameashiria ukomavu wa kisiasa, azma ya kimapinduzi na uhodari wa taifa la Iran katika uchaguzi uliokuwa na hamasa kubwa na wa kusisimua wa Rais wa kumi wa Jamhuri ya Kiislamu na akasema:
Kushiriki kwa zaidi ya asilimia 80 ya wananchi katika zoezi hilo na kura milioni 24 alizopata rais mteule ni sherehe halisi ambayo maadui wanafanya njama za kuharibu tamu yake; Kwa msingi huo wananchi wote hususan tabaka la vijana, wanapaswa kuwa macho kikamilifu. Vilevile amewataka wafuasi wa rais mteule na wagombea wengine kujiepusha na mwenendo na kauli ya aina yoyote ya kichochezi na ya kuzusha dhana mbaya.

Matini ya ujumbe wa Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ni kama ifuatavyo:

Kwa jina la Mwenyezi Mungu Mwingi wa rehma Mwenye kurehemu.

Taifa azizi la Iran!

Enyi wanaume na wanawake werevu, shujaa na wanaotambua zama!

Amani ya Mwenyezi Mungu iwe juu yenu baada ya kuthibitisha kuwa mnastahiki amani na rehma za Mola Mlezi. Ijumaa yenu ya hamasa ilikuwa tukio la kustaajabisha na lisilokuwa na kifani ambalo limedhihirisha upevu wa kisiasa, azma ya kimapinduzi na uwezo na kiraia wa taifa la Iran katika sura nzuri na maridadi mbele ya macho ya walimwengu.

Uwezo na ezi mliosajili katika historia ya nchi hii na irada na azma imara mliyoonyesha kwa mahudhurio yenu makubwa katika zoezi hilo muhimu licha ya moto mkubwa wa vita vya kisaikolojia vya maadui yana umuhimu mkubwa ambao hauwezi kuelezeka kwa matamshi ya kawaida. Jambo pekee la kusema ni kuwa, taifa la Iran limeweza tena kujitayarishia uwanja wa kupata rehma za Mwenyezi Mungu na kubakisha mkono wa uwezo wa Mola unaolinda maendeleo na ustawi wa nchi hii.

Uchaguzi wa rais wa tarehe 12 Juni umeweka rekodi mpya katika silsila ya chaguzi mbalimbali za kitaifa. Kushiriki kwa zaidi ya asilimia thamanini ya wananchi katika zoezi hilo na kura milioni 24 alizopewa rais mteule ni sherehe halisi ambayo kwa uwezo wake Mola, itadhamini maendeleo na ustawi wa nchi, usalama wa taifa na harakati endelevu. Jana mliweza kuthibitisha kwamba, kwa baraka za nara na thamani za Mapinduzi ya Kiislamu, Iran imeweza kuwa imara na kuwa na kinga mbele ya hujuma za kisiasa na kisaikolojia, kwa kadiri kwamba imepata uhai na nguvu mpya na kuwathibitishia marafiki na maadui kwamba itaendeleza mbele njia yake licha ya kupita miaka thalathini sasa tangu kuanza kwa demokrasia ya kidini hapa nchini. Ninasimama kwa heshima mbele ya azma na imani yenu na kutoa salamu za pongezi za mafanikio haya kwa Imam wa zama Mahdi (as), kwa roho ya Imam Khomeini (Mwenyezi Mungu amrehemu) na wananchi wote na ninawausia kuthamini neema hiyo ya Mwenyezi Mungu na kumshukuru Mola Mwenye hikima na Mjuzi wa yote.

Inatazamiwa kuwa madui watafanya harakati za kujaribu kuharibu tamu ya tukio hili. Kwa msingi huo ninawausia wananchi wote hususan tabaka la vijana wapendwa ambao ndio waliokuwa vinara wa tukio hili la kusisimua, kuwa macho kikamilifu. Daima Jumamosi hii ya baada ya uchaguzi inapaswa kutambuliwa kuwa siku ya upendo na uvumilivu. Wafuasi wote wa mgombea aliyeshinda na wagombea wengine wanapaswa kujiepusha na aina yoyote ya mwenendo au matamshi ya kichochezi na ya kuzusha dhana mbaya. Rais wa Jamhuri aliyechaguliwa ni Rais wa taifa zima la Iran na wananchi wote, wakiwemo wapinzani wake wa jana, wanapaswa kumuunga mkono na kumsaidia. Bila shaka huo pia ni mtihani wa Mwenyezi Mungu ambao mafanikio ndani yake yataleta rehma zake Mola Mtukufu.

Ninalazimika kuwashukuru kwa dhati wale wote waliochangia katika kufanikisha tukio hili kubwa. Ninatoa shukrani kwa wagombea ambao wamefanikiwa kwa mijadala yao ya kisiasa na kiuchumi na mienendo na maneno yao, kuwaleta katika medani ya uchaguzi watu wenye mirengo na mitazamo tofauti ya kisiasa na kijamii, wasomi mbao wamewahamasisha wananchi kushiriki katika mtihani huu mkubwa, viongozi na maulamaa wa kidini, wasomi wa vyuo vikuu, shakhsia wa kitamaduni na kisiasa, Shirika la Utangazaji la Taifa na viongozi na wafanyakazi wake ambao wametoa mchango mkubwa katika kufanikisha tukio hilo ambalo halitasahaulika. Vilevile ninatoa shukrani za dhati kwa Wizara ya Mambo ya Ndani, Baraza la Kulinda Katiba ambalo limetekeleza kikamilifu wajibu wake mkubwa kwa ikhlasi na uaminifu, kikosi cha polisi na taasisi nyingine za kulinda amani na usalama ambazo zimetayarisha anga ya wazi na ya utulivu kwa ajili ya wananchi. Hatimaye na zaidi ya yote, ninatoa shukrani za dhati kwa wananchi wote waliopiga kura katika uchaguzi wa Rais ambao wamelinda heshima na usalama wao wenyewe na taifa lao.

Kwa mara nyingine tena ninamshukuru kwa moyo wote na kwa unyenyekevu Mwenyezi Mungu Muweza na kuliombea uongofu na rehma taifa hili na mimi mwenyewe mja dhaifu. Ninatuma salamu kwa Imam wa zama Imam Mahdi (as) nikitarajia dua na uungaji mkono wake yeye ambaye ndiye kiongozi halisi wa nchi hii. Aidha ninatuma salamu kwa roho ya hayati Imam Khomeini na roho za mashahidi watukufu.

Amani ya Mwenyezi Mungu na Rehma zake ziwe juu yenu.

Sayyid Ali Khamenei

23 Khordad 1388

13 Juni 2009

419978
captcha