IQNA

Watoto wa Gaza wang’ara katika Kampeni ya Qur’ani ya ‘Nuur’

17:16 - May 20, 2026
Habari ID: 3482263
IQNA – Katika programu iliyofanyika Gaza, watoto 65 walioshiriki katika kampeni ya Qur’ani ya “Nuur” walisoma sehemu za Qur’ani Tukufu mbele ya walimu wao, kisha wakatunukiwa na kupongezwa na viongozi pamoja na wazazi wao.

Watoto hao 65, wavulana na wasichana wenye umri wa kati ya miaka 4 hadi 9, wakiwa wamevalia mavazi ya jadi ya Kipalestina na mavazi maalumu ya “Wabebaji wa Nuru”, walishiriki katika hafla hiyo iliyofanyika katika shule na chekechea ya Gharas huko Gaza, ambapo walisoma aya na sura mbalimbali za Qur’ani Tukufu mbele ya walimu wao.

Wakiwa wamebeba mabango yaliyobeba ujumbe wa kampeni hiyo wa kupanda mapenzi ya Qur’ani Tukufu nyoyoni, walionesha taswira ya kugusa ya watoto wanaotafuta kuifikia nuru katika nyakati zilizojaa vita, mashinikizo na dhiki.

Katika mkusanyiko huo, uliotawaliwa na hali ya imani na utulivu wa kiroho, nyuso za watoto hao zilidhihirisha bashasha na ari ya pekee. Walimu na wazazi, wakijawa na fahari, walimwaga machozi ya furaha waliposhuhudia wanafunzi na watoto wao wakipiga hatua zao za mwanzo katika njia ya kuhifadhi Kitabu cha Allah.

Mandhari hiyo haikuwa tu kikao cha kawaida cha kuhifadhi na kusoma Qur’ani, bali ilikuwa picha hai ya mtoto ambaye, katikati ya vita na chini ya uzito wa maumivu na mateso yake, alijitahidi kushikamana na nuru ya imani yake na kufikisha ujumbe unaothibitisha kwamba Qur’ani bado ina uwezo wa kufufua matumaini, yakini na utulivu wa moyo katika nyoyo za vijana.

Mpango huo wa kiroho wa “Harakati ya Nuru” uliundwa kwa lengo la kutoa mazingira salama ya malezi na elimu ya Kiimani kwa watoto wa Gaza, ili kujenga mafungamano kati ya kizazi kipya na Qur’ani Tukufu kupitia hifdh, tilawa na uelewa wake, pamoja na kuwasilisha mfano bora wa tabia na mwenendo kwa jamii ya Waislamu wa Palestina.

Maafisa wamesisitiza kwamba kuwaenzi watoto wanaohifadhi Qur’ani hakupimwi tu kwa kiwango cha walichohifadhi, bali pia kwa kujenga mwanadamu anayebeba nuru moyoni mwake, anayekua akiwa na huruma zaidi, uelewa mpana na dhamira thabiti. Huu ni ujumbe unaosisitiza kwamba Qur’ani bado ina uwezo wa kuleta matumaini na uhai hata katika mazingira magumu zaidi.

3497517

Habari zinazohusiana
Kishikizo: gaza qurani tukufu
captcha