
Katika ujumbe huo, rais wa Iran alisisitiza haja ya jumuiya ya kimataifa kuchukua mtazamo wa kweli na wa haki, na akazitaka nchi za dunia kukabiliana na matakwa yasiyo halali pamoja na sera za hatari na za kimajaribio za Marekani.
Ujumbe wa Pezeshkian, kwa mujibu wa tovuti rasmi ya urais wa Iran, ni kama ifuatavyo:
Kwa Jina la Mwenyezi Mungu, Mwingi wa Rehema, Mwenye Kurehemu
“Na ama kina ‘Aad walifanya kiburi katika ardhi bila haki wakasema: Ni nani aliye na nguvu kuliko sisi? Je, hawakuona kwamba Mwenyezi Mungu aliyewaumba ndiye mwenye nguvu zaidi kuliko wao? Nao walikuwa wakizikataa aya Zetu.”
Qur’ani Tukufu, Surah Fussilat, Aya ya 15
“Mwanzo wa kiburi ni pale mtu anapoacha kumtii Mungu na moyo wake unapoelekea mbali na Muumba wake. Kwa maana kiburi ndicho mwanzo wa dhambi, na mwenye kuwa nacho hutoa maovu mengi; na kwa sababu hiyo Bwana aliwaletea maangamizi yasiyotarajiwa na akawaangamiza kabisa.”
Biblia Takatifu, Sirach 10:12–13
Utakatifu Wako Papa Leo XIV
Kiongozi Mwenye Heshima wa Wakatoliki wa Dunia
Ninakupa salamu zangu za dhati na za heshima, na ninatoa shukrani kwa misimamo yako ya kimaadili, ya busara na ya haki kuhusu shambulizi lililofanywa tarehe 28 Februari 2026 na utawala wa Marekani, ambalo kwa mara ya pili na katikati ya mazungumzo kati ya nchi hiyo na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, lilifanywa kwa visingizio visivyo na msingi na kwa ukiukaji wazi wa sheria za kimataifa, kwa ushirikiano na utawala wa Israel.
Kutokana na uchokozi huo usio halali wa Marekani na utawala wa Israel, Kiongozi Mkuu wa ulimwengu wa Kishia, Ayatullah Udhma Imam Sayyid Ali Khamenei, pamoja na idadi kubwa ya maafisa wa juu wa kisiasa na kijeshi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, waliuawa na kufa shahidi. Aidha, raia 3,468 wa Iran, wakiwemo watoto wasio na hatia wa Shule ya Shajareh Tayyebeh katika mji wa Minab, waliuawa shahidi. Pia uharibifu mkubwa ulisababishwa kwa miundombinu yetu, ikiwemo shule, vyuo vikuu, urithi wa kitamaduni na majengo ya kihistoria, vituo vya elimu, maeneo ya ibada kama misikiti na makanisa, vituo vya afya, viwanja vya michezo, hospitali, madaraja, barabara, reli, vituo vya umeme, viwanda vya kusafisha mafuta na mitambo ya petrokemikali, mifano iliyo wazi ya uhalifu wa kivita.
Rais wa Marekani hapo awali alitoa kauli hatari na ya aibu akisema kuwa ananuia kuangamiza ustaarabu wa kihistoria wa Iran na kuirudisha katika enzi za mawe. Kama ulivyobainisha, kauli kama hizi hutokana na dhana potofu ya nguvu kamili na zinatokana na kiburi, uonevu, tamaa ya kupita kiasi, na juhudi za kutatua migogoro kwa kutumia vurugu zisizozuilika, tabia ambayo dhamiri ya kibinadamu haiwezi kuielewa wala kuikubali.
Mtazamo wa uharibifu wa Marekani na utawala wa Israel pamoja na mashambulizi yao yasiyo halali haujaelekezwa dhidi ya Iran pekee, bali pia dhidi ya utawala wa sheria katika ngazi ya kimataifa, sheria za kimataifa, maadili ya kibinadamu, na mafundisho ya dini za mbinguni. Ni wazi kwamba gharama za mtazamo huo hatari zitabebwa na jumuiya nzima ya kimataifa.
Taifa la Iran, likijumuisha Waislamu, Wakristo, Wayahudi na Wazoroasta, limeishi pamoja kwa karne nyingi katika nchi yao ya kale kwa amani na utulivu, na limeendeleza kuishi kwa maelewano na uvumilivu na majirani zake, wakiwemo wale wa pwani za kusini za Ghuba ya Uajemi, kwa misingi ya uhusiano wa kihistoria, kitamaduni na kidini. Hata hivyo, uwepo wa vituo vya kijeshi vya Marekani katika ardhi za nchi za Ghuba ya Uajemi, ambavyo kwa masikitiko vilitumika katika vita vya hivi karibuni kufanya mashambulizi dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, ulilazimisha Vikosi vya Ulinzi vya nchi yangu, katika mfumo wa kujilinda kisheria na kujibu uchokozi, kulenga malengo na maslahi ya washambuliaji ndani ya ardhi za nchi hizo. Hata hivyo, kama historia inavyoshuhudia, hatujawahi kutishia wala kuvamia mamlaka na mipaka ya majirani zetu, na tunaendelea kutafuta uhusiano bora na majirani wote ili kuishi kwa amani, utulivu na ustawi katika eneo hili.
Hali ya sasa katika Mlango wa Hormuz pia ni matokeo ya mashambulizi yasiyo halali ya washambuliaji pamoja na matumizi ya ardhi na anga ya nchi za pwani ya Ghuba ya Uajemi kufanya mashambulizi dhidi ya Iran, pamoja na mzingiro wa baharini uliowekwa dhidi ya Iran na Marekani. Ni wazi kwamba mara tu hali ya sasa ya ukosefu wa usalama itakapotatuliwa, hali ya usafiri wa majini katika Mlango wa Hormuz itarejea katika hali ya kawaida. Iran pia itatekeleza mifumo madhubuti na ya kitaalamu ya ufuatiliaji na udhibiti, ndani ya mfumo wa sheria za kimataifa, ili kuimarisha usalama wa usafiri katika njia hii muhimu ya bahari.
Jamhuri ya Kiislamu ya Iran daima imeonyesha kujitolea kwake kwa diplomasia na suluhisho za amani katika kutatua masuala mbalimbali, ikiwemo katika mazungumzo na utawala wa Marekani. Kwa lengo hilo, licha ya usaliti wa mara kwa mara wa utawala huo dhidi ya mazungumzo na diplomasia, Iran ilikaribisha upatanishi wa Pakistan na imeingia katika mazungumzo ya Islamabad kwa dhati na kwa weledi. Kusimama imara kwa Iran mbele ya matakwa yasiyo halali ya utawala wa Marekani kwa hakika ni utetezi wa sheria za kimataifa na wa maadili ya juu ya kibinadamu. Kwa hiyo, jumuiya ya kimataifa inatarajiwa kuchukua mtazamo wa kweli na wa haki na kukabiliana na matakwa yasiyo halali pamoja na sera za hatari na za kimajaribio za Marekani.
Napenda kwa mara nyingine tena kueleza shukrani za serikali na wananchi wa Iran kwa msimamo wako unaotegemea dhana ya “amani ya haki,” na kusisitiza kwamba Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, huku ikilinda haki yake ya kujitetea kisheria, bado imejizatiti kwa dhati katika mazungumzo na katika kutatua matatizo kwa njia za amani kwa mujibu wa sheria na maadili.
Masoud Pezeshkian
Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran
3497474