
Shule, hospitali, na nyumba zimesawazishwa na ardhi. Hata hivyo, mshumaa wa mapenzi na ikhlasi kwa Kitabu cha Allah haujazimika, badala yake, unazidi kung’ara kwa mwangaza mkali zaidi.
Vita na uharibifu mkubwa ulioachwa nyuma havitoshi kuuzima moto wa mahaba kwa Qur'ani Tukufu, wala kuondoa azma ya kuhifadhi na kujifunza maneno ya Mwenyezi Mungu katika nyoyo za watu wa Gaza.
Licha ya uharibifu mkubwa uliofanywa dhidi ya miundombinu, taasisi za kidini na kielimu, misikiti, na vituo vya kuhifadhia Qur'ani katika kipindi hiki cha miaka miwili ya vita, Ukanda wa Gaza unashuhudia vuguvugu kubwa la kiserikali na kijamii la kufufua vituo vya Qur'ani. Hatua hii inatumika kama nyenzo madhubuti ya uponyaji wa kiroho na kisaikolojia, na katika kuijenga upya rasilimali watu iliyochoshwa na vita hivyo vya kinyama.
Rami al-Shaqra, msimamizi wa Kituo cha Al-Nour cha Kuhifadhi Qur'ani na Sayansi zake katika Ukanda wa Gaza, alisisitiza kuwa kazi ya kituo hicho ni jitihada za kurejesha na kuijenga upya utambulisho wa Kipalestina mbele ya athari za vita na majaribio ya kuhujumu kila nyanja ya maisha.
Alisema kuwa Shule ya Qur'ani ya Al-Nour ilianzishwa juu ya magofu yaliyosababishwa na uharibifu wa wavamizi.
Al-Shaqra aliashiria kuwa lengo la sasa ni “kuijenga upya rasilimali muhimu zaidi, ambayo ni mwanadamu, na kumfinyanga upya mtu aliyechoshwa na vita hivi vya mauti kupitia programu jumuishi ya Qur'ani na malezi.”
Alibainisha kuwa kwa sasa kituo hicho kinavutia takriban wanafunzi 800 wa kiume na kike wa umri tofauti, kuanzia watoto wadogo hadi wazee wenye umri wa zaidi ya miaka 60, ambao wametengewa programu maalum kulingana na umri wao.
Afisa huyo aliongeza kuwa mfumo huu unasimamiwa na wafanyakazi wa malezi na mafunzo wapatao 60, wakiwemo wasimamizi na walimu wa Qur'ani (Maalim).
Kuhusu aina ya programu zinazotolewa kwa wanafunzi katika mazingira haya magumu, al-Shaqra alieleza kuwa programu ya kituo hicho haishishii tu kwenye ibada na hifdhi ya kawaida, bali inatokana na maono mapana ya kielimu na kisaikolojia. Lengo ni kuifanya Qur'ani Tukufu kuwa sehemu ya maisha ya kila siku ya wananchi kama njia ya uponyaji wa nafsi na kuvuka madhara ya kiwewe.
“Mara tu baada ya kusimama kwa mapigano, tuliandaa mitaala jumuishi ya kielimu inayofaa kwa makundi yote ya umri,” alisema.
“Programu hii inajumuisha sehemu muhimu ya kutoa shinikizo za kisaikolojia na kihisia kwa wanafunzi, ikisimamiwa na kundi teule la wanasaikolojia na washauri ili kuijenga upya haiba na nafsi ya mtu,” aliongeza al-Shaqra. “Sambamba na hayo, kuna programu ya elimu inayochunguza kisa za Qur'ani, wasifu wa watu mashuhuri na viongozi wenye ushawishi katika historia ya Kiislamu ili kuuunganisha kizazi hiki na mizizi pamoja na utambulisho wake.”
Abu Shaaban aliliambia Shirika la Habari la Qatar (QNA) kuwa halaka za darsa za Qur'ani zimekuwa kimbilio la amani kwa watoto walioyakimbia makazi yao, zikiwapa utaratibu wa kila siku uliorejesha hali ya utulivu, mbali na kupandikiza maadili ya subira na kupunguza athari ngumu za kitabia zinazosababishwa na kuishi kwa muda mrefu katika kambi za wakimbizi.
Huda al-Farra, mwenye umri wa miaka 56, aliiambia QNA: “Shule hii ya Qur'ani imekuwa kichocheo kikubwa kwetu kuhifadhi Kitabu cha Mwenyezi Mungu na kujifunza fiqhi ya Kiislamu na sayansi za dini.”
“Baada ya yote tuliyovumilia – kupoteza familia na wapendwa wetu, dhuluma, na kufukuzwa makazini – tumepata kimbilio salama katika Kitabu cha Mwenyezi Mungu,” alisema. “Tumepata nguvu na utulivu (sakina) ili tuweze kuanza maisha yetu upya.”
3497381