IQNA

Hujuma ya kigaidi katika Msikiti wa San Diego ni ishara ya mgogoro Chuki Dhidi ya Uislamu Marekani

9:40 - May 22, 2026
Habari ID: 3482267
IQNA – Ingawa hujuma ya kigaidi dhidi ya Msikiti wa San Diefo ilitokea umbali wa zaidi ya maili 2,000, huzuni na taharuki yake zilihisiwa moja kwa moja kote Marekani hadi kusini-mashariki mwa jimbo la Michigan siku ya Jumatano.

Viongozi wa jamii ya Kiislamu kusini-mashariki mwa Michigan wamelaani vikali shambulio lililofanywa wiki hii dhidi ya msikiti mjini San Diego na magaidi wawili vijana, ambao mamlaka zinasema walikuwa wakieneza kauli za itikadi ya ubaguzi wa wazungu wenye misimamo mikali. Viongozi hao walieleza kuwa shambulio hilo ni dalili ya kurejea kwa wimbi jipya la chuki dhidi ya Uislamu (Islamophobia) nchini Marekani.

Magaidi wawili waliotekeleza hujuma hiyo waliotambuliwa na mamlaka za California kuwa na umri wa miaka 17 na 18, walifyatua risasi siku ya Jumatatu katika Kituo cha Kiislamu cha San Diego, California. Watu watatu waliuawa nje ya msikiti huo, miongoni mwao akiwa ni askari wa usalama. Baadaye washambuliaji hao walikutwa wamefariki dunia baada ya kujipiga risasi wenyewe. Polisi wanaendelea kuchunguza hujuma hiyo ya kigaidi kama uhalifu wa chuki, wakisema kuwa “matamshi ya chuki” yalichangia ugaidi huo.

“Kila shambulio dhidi ya nyumba ya ibada ni shambulio dhidi ya misingi ya uhuru wa dini, heshima ya mwanadamu na kuishi kwa amani,” alisema Imam Steve Mustapha Elturk, mwenyekiti mwenza wa Baraza la Maimamu wa Michigan, katika mkutano na waandishi wa habari siku ya Jumatano. Alizungumza akiwa pamoja na wanachama wengine wa Baraza hilo katika Taasisi ya Da‘wah jijini Detroit, pamoja na mgombea wa Seneti ya Marekani, Abdul El-Sayed.

Kundi hilo la viongozi wa Kiislamu limekuwa likitoa matamko mara kadhaa katika miezi ya hivi karibuni kuhusu machafuko ya kivita katika Mashariki ya Kati yaliyosababisha majanga ya kibinadamu na vifo vya raia kwa wingi, ikiwemo mashambulizi ya Marekani na Israel dhidi ya Iran, mashambulizi ya Israel nchini Lebanon, na vita vya mauaji ya kimbari vinavyoendelea Gaza.

Mamlaka zimetambua waliouawa shahidi katika msikiti huo kuwa ni Amin Abdullah, aliyekuwa mlinzi pamoja na Mansour Kazlha na Nadir Awad. Wametajwa kuwa mashujaa kwa kujaribu kuwakabili washambuliaji.

Sayyid Ali Jafri, msomi katika Kituo cha Zainabia cha Michigan, kituo cha kijamii na “nyumba ya kiroho” inayohudumia Waislamu wa eneo la Metro Detroit, aliwaelezea washambuliaji hao wawili walichochewa na matamshi ya chuki na propaganda dhidi ya Uislamu nchini Marekani, yanayoenezwa na baadhi ya wanasiasa na vyombo vya habari.

Alisema kuwa wakati mwingine Marekani imeshindwa kufikia malengo yake ya Kikatiba ya kuimarisha utulivu wa ndani na haki, na kwamba kupanda mbegu za mgawanyiko ni kuwatendea vibaya wananchi wake. Jafri pia ni mkurugenzi wa Dar al-Dhikr, taasisi inayolenga kushirikisha urithi wa kiroho na kielimu wa Uislamu.

“Lakini hili linaendelea kuwa lengo la Waamerika wote—bila kujali rangi yetu, asili yetu, kabila letu au dini yetu, kujitahidi kulifikia,” alisema Jafri.

Mkuu wa Polisi wa San Diego alisema kuwa mama wa mmoja wa vijana hao alipiga simu polisi saa mbili kabla ya shambulio kuripoti kuwa mwanawe amepotea. Bunduki zake pia zilikuwa zimechukuliwa, na mwanzoni alidhani mwanawe alikuwa na nia ya kujiua. Hata hivyo, mamlaka zilianza kushuku mpango hatari zaidi baada ya mama huyo kusema mwanawe alichukua bunduki tatu, akaondoka na rafiki yake, na wote walikuwa wamevalia mavazi ya kijeshi ya kujificha (camouflage).

Shambulio hilo la kigaidi limetokea wiki moja kabla ya sikukuu kubwa ya Kiislamu ya Eid al-Adha, au Sikukuu ya Kuchinja, inayoanza jioni ya Jumatano ijayo, pamoja na msimu wa ibada ya Hija, ambapo mamilioni ya waumini wa Kiislamu huelekea katika Mji Mtakatifu wa Makkah, Saudi Arabia.

El-Sayed alihoji, “Ni aina gani ya itikadi ambayo vijana hawa wamekuwa wakiloweshwa ndani yake” hadi kufikia hatua ya kufyatua risasi msikitini na kisha kukatiza maisha yao wenyewe.

“Lazima tujiulize maswali makubwa kuhusu kwa nini watu wanashambulia maeneo kama haya. Hii inasema nini kuhusu jamii yetu?” alisema El-Sayed. “Ni katika dunia gani, ni katika aina gani ya Amerika, tunawageuza vijana kuwa magaidi?”

El-Sayed anawania kiti cha Seneti ya Marekani kitakachoachwa wazi na Seneta wa Chama cha Democratic, Gary Peters.

3497545

captcha