
Maelfu ya Wapalestina wa Gaza wameshindwa tena kutekeleza ibada ya Hija huku Israel ikiendelea kuweka vikwazo vya usafiri kupitia mipaka ya Gaza.
Wakati Waislamu kutoka pembe zote za dunia wakifika Saudi Arabia kwa ajili ya ibada ambayo ni miongoni mwa nguzo za Uislamu, wengi wa Wapalestina wa Gaza wanasalia wakiwa wamekwama kutokana na vita, mzingiro na ukimbizi.
Kufungwa kwa vituo vya mpakani na janga la kibinadamu lililotokana na vita kumewanyima maelfu ya Wapalestina fursa ya kutekeleza moja ya nguzo muhimu zaidi za dini ya Uislamu.
Shirika la Habari la Anadolu limeangazia kisa cha Suad Hajjaj, mwanamke Mpalestina ambaye maandalizi yake ya miaka mingi kwa ajili ya Hija yameishia katika majonzi makubwa.
Kabla ya vita, Hajjaj alikuwa amesajiliwa kusafiri na mumewe, ndugu yake wa kiume na shemeji yake. Lakini taarifa zinaeleza kuwa mumewe aliuawa katika shambulio la Israel, ndugu yake ametoweka, na nyumba yao iliharibiwa kabisa.
Sasa akiwa amehamishwa na kuishi katika Uwanja wa Yarmouk mashariki mwa Mji wa Gaza, Hajjaj alisema kuwa akiba ya familia iliyokusudiwa kwa safari ya Hija ilizama chini ya vifusi vya nyumba yao. Aliokoka akiwa na watoto wake baada ya kupoteza karibu kila kitu.
Wakati mahujaji wakikusanyika Makkah, Hajjaj ana mazjoni ambayo pia yamehuisha kumbukumbu ya kifo cha mumewe na kusambaratika kwa maisha waliyotarajia kujenga pamoja.
Hajjaj bado ana matumaini kwamba siku moja ataweza kutekeleza Hija.
Rami Abu Staitah, Mkurugenzi Mkuu wa Hija na Umra katika Wizara ya Awqaf na Mambo ya Kidini ya Gaza, alisema kuwa Palestina hupokea mgao wa mahujaji 6,600 kwa mujibu wa makubaliano na Saudi Arabia, na Gaza ikipata takribani asilimia 38 ya nafasi hizo.
Kulingana na Abu Staitah, Wapalestina 2,473 kutoka Gaza walikuwa wamepitia mfumo wa bahati nasibu wa Hija tangu 2013 na walikuwa wakisubiri zamu yao.
Alisema kuwa 71 walifariki kabla ya kufikia safari ya Hija, wengine katika mashambulizi, wengine kwa sababu za kawaida, na 2,402 wanasalia bila uwezo wa kusafiri.
Abu Staitah alieleza kuwa kuendelea kwa hali hii ni “pigo kubwa” kwa Waislamu wa Gaza. Wananchi wengi wanaendelea kuwasiliana na Wizara ya Awqaf kuhakikisha majina yao bado yanasalia kwenye orodha, wakitumaini kuwa siku moja wasafiri wataweza kuruhusiwa.
Kabla ya vita, mahujaji wa Gaza walikuwa wakivuka kupitia mpakani wa Rafah kuelekea Misri, kisha Cairo, na baadaye Saudi Arabia.
Mchakato huo ulihusisha uratibu kati ya viongozi wa kidini wa Kipalestina pamoja na maafisa wa Misri na Saudi Arabia.
Hata hivyo, utawala wa Israel uliteka na kufunga upande wa Kipalestina wa mpakani wa Rafah mnamo Mei 2024, na kuikata Gaza kutoka njia yake ya mwisho ya moja kwa moja kuelekea ulimwengu wa nje.
Ingawa mpakani huo baadaye ulifunguliwa kwa baadhi ya wagonjwa, usafiri wa raia bado unadhibitiwa sana.
Abu Staitah alisema kuwa jitihada zinaendelea kwa kushirikisha wadau wa ndani na kimataifa ili kuwezesha safari, lakini bado zinakumbana na vikwazo vikubwa kutokana na kufungwa kwa mipaka na masharti makali ya usafiri.
Kwa Wapalestina wengi, kushindwa kutekeleza Hija hakumaanishi tu kikwazo cha kiutendaji, bali pia ni sura nyingine ya maumivu ya muda mrefu na hali ya kutokuwa na uhakika chini ya mazingira ya vita na mzingiro unaoongezeka.
3497553