
Sekretarieti Kuu ya OIC imetoa taarfia ikilaanii nia ya kile kinachoitwa “Somaliland” ya kufungua ubalozi mjini al‑Quds, hatua inayotafsiriwa kuwa ishara ya kuongezeka kwa uhusiano kati ya eneo hilo la Pembe ya Afrika na utawala haramu wa Israel.
Sekretarieti Kuu ilieleza katika taarifa yake kwa vyombo vya habari kuwa inatiwa wasiwasi mkubwa na inalaani vikali taarifa za kimitandao kuhusu mpango wa “Somaliland” kufungua kile kinachoitwa “ubalozi” katika mji wa Al Quds unaokaliwa kwa nguvu. Ilisema hatua hiyo ni “ukaidi wa wazi dhidi ya matakwa ya jumuiya nzima ya kimataifa” na “ukiukaji mkubwa wa misingi ya Hati ya Umoja wa Mataifa pamoja na maazimio yake husika.”
Taarifa hiyo iliongeza kuwa hatua hii isiyo halali inaingia katika muktadha wa “jaribio la Israel, lisilo na uhalali, la kutafuta utambuzi wa bandia kutoka kwa taasisi au maeneo yasiyotambuliwa kimataifa, yakiwemo eneo linalojiita ‘Somaliland’, kwa lengo la kuhalalisha madai yake ya utawala juu ya mji wa Al Quds unaokaliwa kwa nguvu, jambo ambalo linakwenda kinyume kabisa na sheria za kimataifa.”
OIC ilisisitiza kuwa “Israel, kama utawala unaokalia kwa mabavu ardhi ya Palestina, hauna mamlaka yoyote juu ya Al Quds , mji mkuu wa Taifa la Palestina, na kwamba hatua zozote zinazolenga kubadilisha hadhi ya kisiasa, kidemografia au kijiografia ya mji huo ni batili na hazina uzito wowote chini ya sheria za kimataifa.”
Jumuiya hiyo ilirejea pia “mshikamano wake kamili na wa dhati na Jamhuri ya Shirikisho la Somalia, pamoja na kuunga mkono bila kuyumba mamlaka ya kitaifa, umoja wa ardhi na usalama wa eneo la Somalia.” Aidha, ilitoa wito kwa mataifa yote duniani “kulaani na kupinga hatua hii isiyo halali, kukataa jaribio lolote la kuipa hadhi ya kimataifa taasisi isiyotambuliwa, na kuishinikiza Israel kuheshimu maazimio ya uhalali wa kimataifa.”
3497548