
Mashindano hayo yakiwakusanya wanafunzi, wazazi, pamoja na wanazuoni na wanaharakati wa kijamii kutoka Tripoli, Akkar na maeneo mbalimbali ya kaskazini mwa Lebanon.
Mwaka huu, mashindano yamepokelewa kwa hamasa ya kipekee, ambapo jumla ya wanafunzi 3,660 wa kike na wa kiume kutoka shule 205 walishiriki. Washiriki walitathminiwa na kamati maalumu 140 zenye wataalamu wa masuala ya Qur’ani, huku waandaaji wakieleza kuwa mwitikio huo unaakisi kuongezeka kwa dhamira ya kulea kizazi kipya kwa misingi ya maadili ya Qur’ani.
Katika hotuba yake kwenye hafla ya kufunga mahafali hiyo ya Qur'ani, Fawaz Omar, Rais wa Jumuiya ya Elimu ya Kiislamu ya Lebanon, alizungumzia mafanikio ya kuandaliwa kwa mara ya 42 mashindano hayo, na kutoa shukrani kwa familia za washiriki kwa juhudi zao za kupandikiza tunu za dini katika malezi ya watoto wao.
Kwa upande wake, Sheikh Mohammed Imam, Mufti wa Akkar, alisisitiza kuwa mashindano hayo ni mfano wa kuigwa katika shughuli za kielimu na kidini, na kwamba ushiriki mpana wa wanafunzi unaonesha nafasi na hadhi yake katika kaskazini mwa Lebanon.
Aliongeza kuwa kuipa Qur’ani kipaumbele ni kulea watu wema na waadilifu wenye uwezo wa kuitumikia nchi yao na kukabiliana na changamoto mbalimbali. Aidha, alibainisha kwamba shindano hilo ni hatua muhimu ya kielimu katika kuunganisha vizazi na Qur’ani Tukufu, kulinda jamii dhidi ya upotovu, na kujenga mradi mpana wa kulea kizazi chenye utambuzi na mshikamano na utambulisho wake wa Kiislamu.
Mwisho wa hafla hiyo, washiriki walitembelea kamati za mitihani zilizopo katika Majma‘a ya Shule za Al‑Iman na kusikiliza visomo vya washindani.
Miongoni mwa mambo yaliyojitokeza mwaka huu ni uzinduzi wa programu ya kielektroniki (aplikeshini) inayowezesha kusikiliza visomo vya washiriki, hatua inayodhihirisha juhudi za kuoanisha huduma za Qur’ani na maendeleo ya teknolojia ya kisasa.
3497523