
Alifariki mnamo Mei 5, 2020, akiwa na umri wa miaka 86, baada ya miongo mingi ya kujitolea katika njia ya Qur'ani Tukufu.
Sheikh Tablawi alikuwa qari mwenye mtindo wa kipekee na anayejulikana sana kama Kiongozi wa Maqarii wa Misri, na alihudumu katika uwanja huu kwa zaidi ya nusu karne.
Alizaliwa Novemba 14, 1934, katika kitongoji cha Mait Aqaba, Mkoa wa Giza. Akiwa na umri wa miaka tisa, tayari alikuwa amehifadhi Qur'ani Tukufu kikamilifu, na umaarufu wake kama qari ukaanza kusikika kwa kasi. Alipofikisha miaka 12, alianza kualikwa katika hafla za kuwaheshimu wazee, viongozi, na familia mashuhuri, akiwa sambamba na maqari maarufu wa redio. Kabla ya kufikisha miaka 15, alikuwa tayari amepewa nafasi ya juu miongoni mwao, bishara njema ambayo babu yake aliwahi kumwambia baba yake ikatimia: kwamba mjukuu wao angekuwa hafidh na qari maarufu wa Qur'ani.
Sheikh Tablawi alishiriki kikamilifu katika majopokazi ya kimataifa ya kuhukumu mashindano ya kuhifadhi Qur'ani na alihukumu mashindano mengi ulimwenguni. Alitunukiwa tuzo ya heshima na mamlaka za Lebanon kwa kutambua mchango wake katika kuhudumia Qur'ani Tukufu.
Mwanawe anasema safari ya baba yake katika ulimwengu wa tilawa ilianza akiwa na umri wa miaka minane, wakati wa sherehe ya Siku ya Mama shuleni kwake. Katika hafla hiyo alisoma aya za Surah Luqman, na hapo ndipo kipaji chake kilipoonekana wazi.
Alikumbuka pia kuwa safari yake ya kwanza ya kimataifa akiwa na baba yake ilikuwa Afrika Kusini mnamo 2006, na akashuhudia mapenzi ya watu ambayo hata yalizidi yale aliyoyazoea nchini Misri.
Alisimulia pia baadhi ya sifa za kibinadamu za Sheikh Tablawi kama vile unyenyekevu wake, utaratibu wake wa kusoma Qur'ani kila wiki, na upole aliokuwa nao licha ya umaarufu wake mkubwa duniani katika fani ya tilawa.
Sheikh Tablawi alijulikana kama mwenye Koo la Dhahabu. Viongozi kutoka mataifa mbalimbali duniani, hata kutoka Vatican, walimwalika rasmi. Alialikwa pia kusoma Qur'ani katika mazishi ya Malkia Zein al‑Sharaf, mama wa Mfalme Hussein wa Jordan; mazishi ya Mfalme Hassan II wa Morocco; na mazishi ya Basil, mwana wa rais wa zamani wa Syria, Hafidh al-Assad. Zaidi ya hayo, alipewa mialiko mingi ya kusoma Qurani mbele ya mamia ya Waumini nchini Ugiriki na Italia.
Umakini wake mkali katika kukilinda na kukiimarisha sauti yake, pamoja na mazoea yake ya kukaa karibu na makarii wakubwa kama Mabwana Rifa’at, Ali Mahmoud, Mohamed Salameh, Saifi, Bahtimi na Mustafa Ismail, maqari mahiri wa redio ya Misri, ulimsaidia sana kukomaa katika sanaa ya tilawa.
Kwa upande wake, Sheikh Tablawi alijitahidi zaidi kuliko makarii wengi kujiunga na Redio ya Qurani. Aliomba mara tisa bila mafanikio, lakini kwa Qadar ya Mwenyezi Mungu, ilikubaliwa katika jaribio la kumi , jambo aliloliona kuwa ni ishara ya kuwa mambo yote yako mikononi mwa Mola.
Katika mahojiano aliwahi kusema kwa huzuni: “Heshima na mapenzi ya watu ni medali ya heshima kwangu; lakini kinachoniumiza ni kwamba hapa Misri mara nyingi wasanii ndio wanaopewa heshima. Nimetunukiwa heshima katika nchi nyingi kama Jordan, Saudi Arabia na Lebanon, lakini sijawahi kupewa heshima kama hiyo katika nchi yangu.”
Hatimaye, Wizara ya Awqaf ya Misri ilimheshimu rasmi katika hafla ya kufunga Mashindano ya 23 ya Kimataifa ya Kusoma Qurani yaliyofanyika Sharm El-Sheikh, kwa kumweka katika kiwango sawa na maqari mashuhuri kama Sheikh Mahmoud Khalil al‑Husari na Sheikh Abdul Baset Abdul Samad.
Sheikh Tablawi alisafiri katika zaidi ya nchi 100, lakini safari ambayo daima itabaki moyoni mwake ni ile ya kwenda Saudi Arabia ambapo alisoma Qur'ani Tukufu ndani ya Ukuta wa Kaaba kabla ya adhana, na alikuwa qari pekee duniani kupewa heshima hiyo.
Siku ya kufariki kwake, kituo cha kufundisha wahifadhi wa Qur'ani kilipewa jina lake.
Video iliyo hapa chini inaonyesha Sheikh Muhammad Mahmoud Tablawi akisoma Surah Yunus, aya za 84 hadi 86.
3497382