Vyombo vya usalama vinaendelea na juhudi za kuzuia watu wasiokuwa na vibali vya Hija kuingia au kukaa katika mji wa Makkah na maeneo matakatifu, vikionya kwamba wanaokiuka sheria hizo pamoja na wanaowasaidia watakamatwa na kukabiliwa na hatua za kisheria.
Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Saudia (SPA), polisi wa Makkah hivi karibuni waliwakamata wakazi 18 wenye uraia wa Afghanistan na Pakistan kwa kughushi vibali vya ukaazi, kadi za Nusuk na bangili maalumu za Hija.
Doria za usalama katika mji huo pia zilimkamata mkazi mmoja wa Indonesia aliyekuwa akitangaza huduma za Hija za udanganyifu kupitia mitandao ya kijamii na kupatikana na kadi bandia za Hija.
Katika tukio jingine, vikosi vya usalama vya Hija viliwakamata wakazi watano wa Afghanistan baada ya kukiuka kanuni za Hija kwa kujaribu kuingia Makkah kwa miguu kupitia eneo la jangwa bila kibali.
Aidha, vikosi hivyo viliwakamata wakazi 10 wenye uraia wa Sudan, Misri na Yemen kwa kukiuka kanuni za Hija kwa kujaribu kuingia na kubaki katika mji wa Makkah bila vibali halali.
Hatua za kisheria zimechukuliwa dhidi ya wote waliokamatwa na kesi zao kuwasilishwa kwa Mamlaka ya Mashtaka ya Umma, kwa mujibu wa SPA.
Kabla ya kuanza kwa msimu wa Hija, Wizara ya Mambo ya Ndani ya Saudi Arabia ilitangaza faini zinazokadiriwa kati ya riyali 20,000 hadi 100,000 za Saudi (takribani dola 5,330 hadi 26,660) kwa yeyote atakayekiuka kanuni za Hija.
Wizara hiyo imesisitiza wito wake kwa raia, wakazi na wenye visa kufuata kikamilifu kanuni za Hija na kuepuka adhabu za kisheria, ikikumbusha kuwa kupata kibali halali cha Hija ni sharti la lazima.
Pia imewahimiza wote kuzingatia taratibu zilizowekwa na kushirikiana na mamlaka husika ili kuhakikisha usalama na utulivu wa mahujaji katika ibada hiyo tukufu.
3497399