
Katika hotuba yake ya televisheni iliyorushwa moja kwa moja kutoka mji mkuu wa Yemen, Sana’a, siku ya Jumatatu jioni kuadhimisha kuingia kwa mwezi mtukufu wa Dhul-Hijjah, Sayyid Abdul-Malik al-Houthi ametoa wito kwa nchi za Kiislamu kusimama imara kukabiliana na njama na uchokozi wa maadui, hususan kupitia vikwazo vya kiuchumi na kisiasa.
Amesema kuwa kuna njia nyingi ambazo matabaka mbalimbali ya ulimwengu wa Kiislamu, yakiwemo serikali, makundi ya kisiasa, na mataifa kwa ujumla, yanaweza kuzitumia ili kufikia lengo hilo.
“Vikwazo vya kiuchumi na kisiasa vina nguvu kubwa sana, na vinaweza kuweka shinikizo lisilovumilika kwa maadui. Ulimwengu mzima umeathiriwa na kushindwa kwa Marekani katika vita vyake vya hivi karibuni vya uchokozi dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, kwani bei za mafuta bado hazijatulia katika masoko ya kimataifa. Hebu fikiria nini kingetokea ikiwa nchi za Kiislamu zitaamua kuweka vikwazo (dhidi ya maadui),” alisisitiza Al-Houthi.
Kiongozi huyo wa Ansarullah amesikitishwa na ukweli kwamba sehemu kubwa ya serikali za nchi za Kiislamu hazina azma na ujasiri wa kutosha kuchukua msimamo thabiti, akionya kuhusu madhara makubwa ya udhaifu huo.
Alibainisha kuwa Uzayuni, pamoja na tawala za Marekani na Israel, ndio maadui wakuu, wakali zaidi, na wasioweza kusuluhishika dhidi ya Waislamu wote.
Katika sehemu nyingine ya hotuba yake, Al-Houthi alilaani vikali kimya cha viongozi wa nchi za Kiarabu na Kiislamu mbele ya ukatili na dhulma za utawala wa Israel dhidi ya Wapalestina katika Ukanda wa Gaza.
Kiongozi huyo wa Ansarullah amesisitiza kuwa serikali za nchi za Kiarabu na Kiislamu zina wajibu wa kidini na kimaadili wa kuwapa silaha Wapalestina, ili taifa hilo linalodhulumiwa liweze kujilinda dhidi ya majeshi ya Israel na walowezi haramu wenye itikadi kali.
Aidha, Al-Houthi aliusifu harakati ya Muqawama ya Hizbullah ya Lebanon kwa kutetea kwa ufanisi na ushujaa ardhi ya Lebanon dhidi ya uchokozi wa mara kwa mara wa Israel.
Kiongozi huyo wa Ansarullah amesema pia kuwa baadhi ya tawala za Kiarabu zinajipanga na kuoanisha maslahi yao na yale ya Marekani na utawala wa Kizayuni.
“Kwa masikitiko, baadhi ya tawala za Kiarabu zimeshindwa kujifunza kutokana na hatari za kuruhusu kambi za kijeshi za Marekani katika ardhi yao,” alisema Al-Houthi.
Mwisho, kiongozi huyo wa Ansarullah aliwashauri watu wa mataifa ya Kiarabu katika kanda hiyo kuwa waangalifu sana mbele ya njama na hila za Marekani na Israel.
3497511